Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI ya Mkoa wa Dodoma imevitaka vikundi vinavyokopeshwa mikopo ya asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani na kukaidi kurudisha mikopo hiyo kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake ili marejesho hayo yaweze kunufaisha wananchi wengi zaidi.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akihutubia katika hafla ya kukabidhi mfano wa hundi ya shilingi 1,389,552,700 kwa vikundi 102 vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma tukio lililofanyika katika bustani ya mapumziko ya Chinangali katikati ya Jiji la Dodoma.
Senyamule alisema kuwa fedha hizi zinazokopeshwa ni nyingi, changamoto ni kiwango cha urejeshaji. “Fedha hizi kila mtu aziheshimu na kuzitumia kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa. Sheria inaruhusu mtu ambae hajarudisha mkopo kushitakiwa mahakamani. Tukaze kidogo ili watu wajue fedha hii si ya kuchezea. Wasiolipa washitakiwe mahakamani ili haki itendeke. Ndugu zangu fedha hizi siyo zawadi ni mkopo, dawa ya mkopo ni kulipa” alisema Senyamule.
Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza sheria. “Pongezi kwa kutoa fedha nyingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Bado zipo halmashauri nyingi hazitoa fedha kwa mujibu wa sheria. Hii ni dhamira ya watu makini ndiyo maana fedha hizi zinatoka hapa Jiji la Dodoma. Nimefahamishwa kuwa mmepewa mafunzo ya kutosha ya mikopo hii isiyo na riba wala masharti. Sharti lililopo ni moja tu, wewe kufanya marejesho, timizeni wajibu wenu” alisema Senyamule.
Aidha, aliziagiza halmashauri za Mkoa wa Dodoma ambazo hazijatoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kutoa mikopo hiyo kwa mujibu wa sheria. Alisema kuwa dhamira ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha wananchi wasio na uwezo wa kukopa katika taasisi za kifedha wapate fursa ya kukopeshwa.
Akiwasilisha taarifa ya utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha Julai-Septemba, 2022 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa jumla ya shilingi 1,389,552,700 zimekopeshwa wa vikundi. “Baada ya uchambuzi, jumla ya vikundi 102 viliidhinishwa kupewa mikopo yenye thamani ya shilingi 1,389,552,700 ambapo vikundi 46 vya wanawake vimekopeshwa shilingi 501,000,000, vikundi 33 vya vijana vimekopeshwa shilingi 693,294,100 na vikundi 23 vya watu wenye ulemavu vimekopeshwa shilingi 195,258,600” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Kwa upande wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jamal Ngalya alimtaja Mkuu wa Mkoa kuwa wa kwanza nchini kukabidhi kiwango kikubwa cha fedha za mikopo ya mapato ya ndani ya halmashauri. Aliwataka vijana kutumia mikopo hiyo kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa. “Kwa vijana tunawaamini, tunawapa fedha za kutosha naomba msituangushe. Hivyohivyo, kina mama sijawataja sana kwa sababu sina mashaka na nyie. Mwakani tukiwa madarakani tutaomba mara mbili ya hizi fedha” alisema Ngalya.
Naye Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Dodoma, Fatma Tawfiq alisema kuwa mikopo hiyo inawasaidia sana wananchi. “Niwapongeze sana Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani. Naamini wote hawa ni waaminifu na watarejesha mikopo hii. Pongezi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri unayoifanya na sisi bungeni tunalitambua hili na tuna kila sababu ya kukupongeza na kukutakia heri” alisema Tawfiq.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.