MWENYEKITI wa Jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma, Billy Chidabwa ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwawezesha vijana kupitia asilimia nne ya mapato yake ya ndani inayotolewa kwa ajili ya mikopo kwa kundi hilo.
Alisema hayo katika ziara iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ilani juu ya asilimia nne ambapo walitembelea vikundi vitatu vya vijana ambao wanafanya ujasiriamali waliowezeshwa kwa mikopo ya Halmashauri na kuendeleza huku wakiwapatia ajira na vijana wengine ambao wako mitaani.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang'anya aliiongoza kamati ya utekelezaji ya Mkoa wa Dodoma katika miradi mitatu inayosimamiwa na vijana jijini hapo ikiwa ni pamoja na miradi wa utengenezaji wa majiko, kilimo cha kisasa cha nyanya pamoja na mgahawa wa chakula na vinywaji ambavyo vyote vinasimamiwa na vijana wabunifu waliowezeshwa kwa kupewa mkopo na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
"Vijana ni nguvu kazi ya taifa la sasa na lijalo, naipongeza Halmashauri ya Jiji hili hasa Mkurugenzi ambaye ni msimamizi na kiongozi kijana Godwin Kunambi kwa kujali vijana na kuwawezesha katika kuwa imara kiuchumi, vijana wengi wana ndoto kubwa lakini wanakwama kutokana na kukosa mitaji ya kuonesha walichonacho.
"Nimejionea miradi mingi na mizuri, badala ya vijana kuilalamikia Serikali kuhusu masuala ya ajira wao wamekuwa wa kwanza kutengeneza ajira kwa wenzao, mfano mzuri ni kikundi cha Youth Enterpreneurship ambao ni wadogo sana lakini wanachokifanya ni kikubwa na wanasaidia na watu wengine kujipatia kipato kwa kuwasambazia majiko wanayotengeneza", alisema Chidabwa.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji alieleza namna ambavyo vijana wamekuwa wathubutu ambapo kati ya vikundi vitatu vilivyotembelewa na kamati hiyo ni vijana wahitimu wa shahada katika fani tofauti walioungana na kuendeleza ujasiriamali kwa upande wa huduma ya vyakula na vinywaji, ambao mbali na ujasiriamali huo wapo na wazo ambalo wanalifanyia kazi katika kuwawezesha vijana wenzao.
"Vijana wakipewa nafasi wana vitu vingi vya kuweza kufanya, mfano hawa wa wajasiriamali wanauza chakula, Tanzania Wazalendo Youth Group wamekuja na mpango kazi wa vijana wengine, lakini wameniletea wazo ambalo kwa akili ya kawaida huwezi kulifikiria, wanatarajia kufanya kongamano la uhamasishaji kwa vijana wenzao, linaloitwa "Great Minds Event" hivyo tujitahidi kuwasapoti kwa kadri tutakavyojaliwa, waweze kufanikisha ndoto walizonazo", alisema Nabalang'anya.
Ziara hiyo ilihusisha jumuiya ya siasa ya vijana Mkoa, walifika na kujionea shughuli zinazofanywa na vijana wathubutu, ambao wamewezeshwa kwa kupatiwa mikopo na Halmashauri ili kuweza kuendeleza ujuzi walionao katika maeneo yao ya kazi, ikiwa ni katika kikundi cha Wanana, Youth Enterpreneurship, pamoja na Tanzania Wazalendo Youth Group.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.