Na. Nancy Kivuyo, MAKUTUPORA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 yanufaisha makundi ya wanawake katika kujikwamua kiuchumi katika Kata ya Makutupora ikitajwa kuwa chachu ya kuinua maendeleo katika sekta ya kilimo, ufugaji na ujasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na makundi ya wanawake waliopata mikopo ya asilimia 10 katika Kata ya Makutupora, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Makutupora, Andrew Boma alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kusimamia vema uwezeshaji wa wananchi kupata haki zao hasa kwa makundi maalum ambayo yamewezeshwa kupitia mikopo hiyo. “Sisi Kata ya Makutupora vikundi 20 vimepatiwa mkopo wa jumla ya shilingi 230,000,000. Vikundi vya wanawake ni 10, vijana saba na watu wenye ulemavu vitatu. Mpaka sasa wameweza kurejesha shilingi 159, 980,000 na bakaa inaendelea kulipwa na vikundi hivyo” alisema Boma.
Aliongeza kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na shughuli mbalimbali kama useremala, ushonaji, ufundi ‘welding’ na biashara ya bodaboda ambazo zinawawezesha kuongeza kipato na kumudu gharama za maisha. “Kimsingi tunamshukuru sana rais wetu kwasababu ameweza kugusa maisha ya watu wenye uhitaji. Mikopo hii imesaidia wananchi kuongeza kipato, kununua mahitaji ya watoto, kununua mali kama viwanja, kumudu gharama za matibabu na kuendesha maisha yao. Kiujumla serikali, mheshimiwa mbunge na diwani nao wana mchango mkubwa sana kwasababu wamekuwa wakitusemea huko kwenye vikao na kufanya umoja wao kuwa na mabadiliko chanya kwa jamii ya Makutupora” aliongeza Boma.
Alisema kuwa anawajibu wa kuhakikisha shughuli za maendeleo katika kata hiyo zinakuwa na mafanikio kupitia elimu na uhamasishaji. “Kiukweli maendeleo ya jamii ni muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla. Mimi hapa Kata ya Makutupora hakuna eneo naweza kulikwepa, kwasababu mambo yote ya msingi yanayomgusa na kumjenga mwananchi nayahudumia kwa kushirikiana na watalaam wengine” alieleza Boma.
Nae, Afisa Mtendaji wa Kata ya Makutupora, Hamisi Jigwa alisema kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa mkombozi kwa wananchi wa Makutupora. “Tunaipongeza sana serikali kupitia rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyajali makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kupitia mikopo hiyo, wanavikundi wamepata faida ambayo inawasaidia kulipa ada za watoto, kununua mahitaji na wengine wamefikia hatua ya kuanzisha miradi mingine iliyotokana na faida. Kwahiyo, niwaase watu wenye uhitaji wa mikopo watembelee ofisi za kata watapata maelekezo namna mikopo hiyo inavyopatikana” alisema Jigwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.