Watumishi mkoani Geita wameshauriwa kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kujenga na kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ally Mketo alipokuwa akifungua kikao baina ya watumishi wa Mkoa wa Geita na wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma waliotembelea Mkoa huo kuelezea fursa za uwekezaji zinazopatikana Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mketo alisema “timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma karibuni sana Mkoa wa Geita, mpo sehemu salama. Watumishi wa Mkoa wa Geita wana ari ya kufahamu Jiji la Dodoma lina fursa gani ili waweze kunufaika nazo”. Alisema kuwa fursa zinapatikana kwa nadra, na kuwashauri kutumia nafasi hiyo kwa manufaa ya uwekezaji na kukuza kipato chao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Afisa Menejimenti Fedha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Felix Mabula alisema kuwa fursa za uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni jambo la msingi ambalo linatakiwa kuwanufaisha watanzania wote. “Fursa za viwanja mara nyingi unapokuwa kijana unahisi hazikuhusu, umri unaposogea ukija kutahamaki unajikuta umechelewa na kuanza kulalamika” alisema Mabula.
Akiwasilisha mada juu ya mipango na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mchumi katika Halmashauri hiyo, Fred Robert alisema kuwa fursa za uwekezaji haziwatengi watumishi wa umma na wawekezaji wengine. “Uwekezaji ni uendeshaji wa uchumi, hivyo kila mtu ana haki sawa katika kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Jiji la Dodoma” alisema Robert.
Akiongelea fursa zilizoainishwa kutoka katika Mpango Kabambe wa Halmashauri hiyo, Robert alizitaja kuwa ni uwekezaji katika maeneo ya elimu, afya, biashara, kilimo na burudani. “Fursa zipo katika uwekezaji wa ujenzi wa vyuo na shule. Maeneo menginge ni ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati” alisema Robert.
Akiongelea fursa za uwekezaji katika biashara, alizitaja kuwa ni uwekezaji katika ujenzi wa viwanda, hoteli, na maduka makubwa. “Halmashauri pia imetenga maeneo kwa ajili ya kilimo cha Kisasa na maeneo ya kuweka ranchi” alisema Robert.
Akiongelea urahisi wa kuwekeza katika Jiji la Dodoma, Robert alisema kuwa Jiji hilo lina maeneo yaliyopangwa na miundombinu iliyosanifiwa vizuri na hakuna msongamano wa magari kutokana na kuwepo kwa mpangilio mzuri wa mfumo wa barabara. “Gharama za kutwaa ardhi ni nafuu na ni rahisi kupata hati milki za ardhi kutoka Halmashauri ya Jiji na kuna wepesi katika kuidhinishiwa ramani na vibali vya ujenzi” alisema.
Nyingine ni uwepo wa rasilimali ardhi ya kutosha na hali ya hewa nzuri. Jiji hilo lipo katika eneo la kimkakati kwa uwekezaji likifikika kirahisi na kupitiwa na barabara kuu (the Great North) inayounganisha miji ya Johannesburg (Afrika Kusini) na Cairo (Misri).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.