Wahisani kutoka Shirika la ABBOT wametoa kiasi cha shilingi milioni 235.9 kwaajili ya ukarabati wa jengo la Zahanati ya Ihumwa, lengo likiwa kuboresha huduma za afya hasa huduma za dharura ambazo zinaenda kupunguza vifo vya wagonjwa mahututi/ majeruhi katika kata hiyo.
Hayo aliyasema Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Andrew Method alipokuwa akisoma taarifa ya mradi mbele ya Kamati ya Fedha na Utawala walipofanya ziara ya kukagua mradi huo.
Dkt. Method alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia zaidi ya wakazi 24112 wa Kata ya Ihumwa na kata jirani pia utapunguza idadi ya vifo vinavyotokana na wagonjwa mahututi kwa kusogeza huduma za dharura karibu zaidi na wananchi.
“Tunashukuru Shirika la Wahisani ABBOT kwa kutoa fedha kwaajili ya kuimarisha miundombinu ya afya katika Zahanati ya Ihumwa. Serikali na washirika wake baada ya kuona huduma za dharura katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbli na zimeonesha matokeo chanya katika kuokoa maisha, ikaona ni busara huduma hii kuanzishwa kwenye ngazi ya zahanati. Katika awamu hii zahanati mbili na kituo cha afya kimoja zinatarajia kuanzisha huduma hii hivyo, kuifanya Zahanati ya ihumwa kuwa moja kati ya zahanati zitakazotoa huduma ya dharura” alisema Dkt. Method.
Kwaupande wake Diwani Neema Mwaluko, Mjumbe kutoka Kamati ya Fedha na Utawala alilipongeza Shirika la ABBOT kwa fedha walizotoa kwaajili ya ukarabati wa zahanati hiyo na kuiomba Kamati ya Fedha na Utawala iridhie kupokea changamoto zilizosomwa kwenye taarifa na kuzifanyia kazi.
“Daktari ametwambia ujenzi huu hautahusisha ujenzi wa uzio, ujenzi wa vyoo vya nje wala uwekaji wa vigae vya chini. Wenzetu wametusaidia nasisi tunatakiwa kuweka mkono kuhakikisha zahanati hii inakamilika kwa ubora unaotakiwa, hii zahanati ni yakwetu inaenda kuhudumia wananchi wetu tusimamie kwa ukaribu kuhakikisha changamoto zinatatuliwa” alisema Diwani Mwaluko.
Naye Diwani Elis Kitendya, Mjumbe kutoka Kamati ya Fedha na Utawala alishauri kujengwe kisima kwenye eneo la mradi sababu miradi mingi inakamilika ila maji yamekuwa ni changamoto kubwa. “Zahanati hii inakwenda kuhudumia maelfu ya wananchi bila kuwa na maji ya uhakika tutajikuta tunazalisha magonjwa mengine ya mlipuko. Tuhakikishe tunaweka miundombinu ya maji sawa hasa kuchimba kisima ili kutatua shida ya maji” alimalizia Kitendya.
Mradi wa Ukarabati wa Jengo la Zahanati ya Ihumwa ulianza tarehe 10/08/2023 unatarajiwa kukamilika tarehe 28/12/2023, ukigharimu kiasi cha shilingi milioni 235.9 fedha kutoka Shirika la Wahisani ABBOT.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.