Na. Coletha Charles, KIZOTA
WANANCHI wa Kata ya Kizota, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanufaika na mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kizota kilichogharimu kiasi cha shilingi 500,000,000.
Diwani wa Kata ya Kizota, Jamal Ngallya alisema kuwa kukamilika kwa kituo hicho kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 500, kitaboresha kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kizota na maeneo Jirani. Kituo hicho kinachojumuisha majengo ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia mamia ya wananchi kwa siku na kuwaepushia kutembea umbali mrefu, alisema.
Katika hatua nyingine aliongeza kuwa majengo yaliyojengwa katika kituo hicho ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mionzi, jengo la huduma ya mama na mtoto, jengo la maabara, kichomea taka, na yataongezwa majengo mengine kama wodi za wagonjwa pamoja na jengo la kuhifadhia maiti.
Alisema kuwa Kituo cha Afya Kizota ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi vya afya jijini Dodoma kwa sasa, na kinatarajiwa kuwa cha tatu kwa ukubwa mara baada ya Makole na Ipagala. “Kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, tumepata kituo cha afya chenye majengo muhimu na ya kisasa. Hili ni jambo ambalo linaongeza hadhi ya kata yetu na linatoa fursa ya kupata huduma bora kwa karibu. Zaidi ya shilingi milioni 500 zimetumika, jambo ambalo linaonyesha jinsi Serikali ilivyojikita katika kuboresha huduma za msingi,” alisema Ngallya.
Nae, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Relini, Lizi Edward, alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho umeondoa adha kubwa iliyokuwa ikiwakumba wakazi, hasa akinamama wajawazito waliokuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za uzazi na vipimo muhimu. “Kipekee sana tunaishukuru serikali kwa ajili ya kutupatia mradi huu wa kituo cha afya. Kupitia kituo hiki watu wengi watakuja kupata huduma. Kwa sasa, kina mama hawahitaji tena kuamka alfajiri au kulazimika kupanda usafiri wa mbali kutafuta huduma. Hii ni nafuu kubwa kwa familia nyingi,” alisema Edward.
Kwa upande wake, Mkazi wa Mtaa wa Relini, Yohana Richard aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajengea kituo cha afya katika mtaa huo, na kusema kuwa ni neema kubwa kwa wakazi wa eneo hilo. “Kabla ya kituo hiki, tulikuwa tunahangaika sana. Tumeenda Makole, ‘General Hospital’, na wakati mwingine hadi Ntyuka kutafuta huduma za afya. Lakini sasa, ndani ya miaka minne tu ya uongozi wa Mama Samia, tumefanikishiwa na tunajivunia kuona huduma hizi muhimu zinakuja karibu nasi na tunaimani tutaletewa madaktari bingwa. Tunaamini tutapata huduma nyingi zaidi na hatutahangaika tena kama zamani,” alisema Richard.
Hata hivyo, Mkazi wa Mtaa wa Relini, Secilia Chundu alisema kuwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kizota umetoa faida kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, kwa upande wa huduma za afya na katika kuongeza ajira na kuinua hali ya kiuchumi ya wananchi, hasa vijana na wanawake. “Ninawashukuru sana viongozi wetu, akiwemo Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge wetu Antony Mavunde, na Diwani wetu Jamal Ngallya kwa kutuletea mradi huu mkubwa. Vijana wetu walipata ajira wakati ujenzi unaanza, wakina mama wajasiriamali walinufaika. Na sasa bado tunatarajia kunufaika zaidi, hasa sisi kina mama tutakuwa na sehemu salama ya kujifungulia karibu na nyumbani. Awali tulikuwa tunahangaika sana, tulikuwa hatuna kituo cha afya kabisa hapa kata yetu, tulilazimika kwenda mbali kufuata huduma” alisema Chundu.
Ujenzi wa kituo hicho umetatua changamoto ya huduma za afya, na umefungua milango kwa uwepo wa ajira kwa watoa huduma na kuimarisha uchumi wa ndani kupitia shughuli ndogo zinazozunguka kituo hicho.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.