Na. Dennis Gondwe, MKONZE
RAIS, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha shilingi 544,225,626 kujenga Shule mpya ya Sekondari Michese ili kupunguza msongamano katika Shule ya Sekondari Mkonze na kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu.
Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Fredrick Mwakisambwe alipoongoza waandishi wa habari kutembelea Shule mpya ya Sekondari Michese iliyojengwa katika Kata ya Mkonze jijini Dodoma.
Mwl. Mwakisambwe ambae ni Afisa Elimu Vifaa na Takwimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “ndugu waandishi wa habari, tupo Kata ya Mkonze eneo la Michese. Eneo hili ni moja ya maeneo yaliyonufaika na kujengwa shule mpya ya sekondari. Kata ya Mkonze ina idadi kubwa ya wananchi na kwa muda mrefu ilikuwa na shule moja ya sekondari ya kata. Mwaka huu 2024 idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika kata ilikua ni wanafunzi 700. Idadi hiyo ni kubwa kuhudumiwa kwenye shule moja ya Sekondari Mkonze. Hivyo, serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kutuletea fedha shilingi 544,225,626 kujenga majengo haya yanayoonekana mazuri na ya kisasa. Madarasa nane, Maabara tatu, jengo la maktaba, jengo la Tehama, jengo la utawala na matundu ya vyoo”.
Alisema kuwa shule hiyo itasaidia mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi na kufundishia kwa walimu. “Kwa kipekee kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na halmashauri tunashukuru sana juhudi hizi na watoto watasoma katika shule hii kwa umbali usio mrefu sana. Tunaipongeza sana serikali kwa uwekezaji huu mkubwa. Na sisi tunaahidi kusimamia taaluma katika Jiji la Dodoma ili juhudi hizi tusimuangushe mheshimiwa Rais” alisema Mwl. Mwakisambwe kwa kujiamini.
Msimamizi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Michese, ambae ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkonze, Mwl. Andrew Rumishael alisema kuwa Kata ya Mkonze ni kubwa ilihitaji shule mpya muda mrefu kwa sababu iliyopo ilizidiwa wingi wa wanafunzi. “Kulikuwa na idadi kubwa sana ya wanafunzi wanaoishi Michese waliokuwa wakitembelea kuifuata Shule ya Sekondari Mkonze. Shule hii itapunguza umbali wa karibu kilomita nane walizokuwa wakitembea wanafunzi kwenda na kurudi na kufanya wawe na nguvu ya kutulia na kusoma vizuri na hata ufaulu wao utaongezeka kwa sababu ya kupunguza umbali huo wa kutembea” alisema Mwl. Rumishael.
Aliongeza kuwa shule hiyo itasaidia kumlinda mtoto wa kike kumaliza masomo yake dhidi ya changamoto za mimba. “Shule hii itamsaidia mtoto wa kike kuzingatia masomo yake na kufikia malengo yake. Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kujali elimu na kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha anatimiza malengo yake” alisema Mwl. Rumishael.
Kwa upande wa mkazi wa Michese Isaya Halwa alipongeza maono ya Rais ya kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Hapo awali watoto wetu walikuwa wanasoma mbali na na elimu ilikuwa shida sana. Tunamshukuru Mungu sababu ya maono na kujituma kwake kuanngalia mazingira ya wananchi wanachohitaji. Mheshimiwa Rais ameona aanze kuandaa kizazi bora cha kesho, sasa tunaona mwanga ambao hatukuwa tukiuona hapo awali” alimalizia Halwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.