Na. Dennis Gondwe, MNADANI
MIRADI ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Dodoma imesaidia kuzalisha ajira na kukuza mzunguko wa fedha kwa wananchi na kuwaletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Godwin Gondwe (aliyesimama pichani juu) katika maelezo yake ya awali kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mtaa wa Mbwanga, Kata ya Mnadani jijini Dodoma eneo inapojengwa shule mpya ya msingi Mbwanga.
Gondwe alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inaleta miradi mingi ya maendeleo katika Wilaya ya Dodoma. Halmashauri ya Jiji imepokea shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya miradi ya BOOST. Hapa Mbwanga shilingi 318,800,000 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya. “Jambo kubwa miradi hii imetusaidia sana kutoa ajira katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Mama lishe wanapika chakula na kuuza kwa mafundi. Mafundi na mafunzi wasaidizi wanapata ajira za ujenzi hapa. Wauza mbao na saruji wanapata biashara kupitia miradi hii. Wauza nondo wanapata biashara na ajira kwenye miradi hii. Miradi hii inakuza mzunguko wa fedha katika Jiji la Dodoma” alisema Gondwe.
Kaimu Mkuu wa Wilaya huyo ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi alifurahishwa na ushiriki wa wananchi wa Mbwanga baada ya Serikali kutoa shilingi 318,800,000 za ujenzi wa shule mpya. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, naomba niwapongeze wananchi wa Mtaa wa Mbwanga sababu wamemuunga mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kusikia mradi huu. Wananchi wenyewe walisafisha eneo na wakapanda miti kuzunguka eneo hili kwa lengo la kulinda mipaka” alisema Gondwe.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akiambatana na kamati yake ya Usalama alifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya elimu katika Jiji la Dodoma akianzia Shule ya Sekondari Bunge, Shule ya Msingi Kisasa, Shule ya Msingi mpya Swaswa inayojengwa na Shule ya Msingi mpya Mbwanga inayojengwa na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo na kufanya mkutano wa hadhara kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Mnadani.
Baadhi ya wanachi wa eneo la Mbwanga wakimsikiliza Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Godwin Gondwe (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Mary Senyamule.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.