UJENZI wa miradi ya kimkakati unaondelea katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma upo katika hatua nzuri ya ukamilishaji wake ili iweze kutumiwa na wananchi na kuongeza mapato ya serikali.
Kauli hiyo ilitolewa na mratibu wa miradi ya kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhandisi Emmanuel Manyanga alipokuwa akiongea na timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga waliotembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujifunza utekelezaji wa miradi ya kimkakati jana jijini hapa.
Mhandisi Manyanga alisema “hali ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ni nzuri. Kama tulivyoona asilimia kubwa ya ujenzi wa barabara zetu zimekamilika na tupo kwenye hatua ya umaliziaji mdogo. Asilimia 95 ya mradi wetu katika barabara umekamilika”.
Mratibu huyo alisema kuwa miradi ya barabara, mitaro ya maji ya mvua na stendi ya malori ya Nala inatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi Disemba, 2019. Akiongelea ujenzi wa mtandao wa barabara uliokamilika, “kwenye stendi ya malori mtandao wa barabara km 26.7 zimekamilika. Mtaro wa maji ya mvua km 6.7, na vivuko sita ambavyo vimeshakamilika pia” aliongeza Mhandisi Manyanga.
“Tunaamini matokeo chanya yanakwenda kuonekana katika miradi hii. Wananchi wanakwenda kufurahia. Tunatarajia miradi hii inakwenda kuleta tija katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na uchumi utaenda kukua kwa kasi” alisema Mratibu huyo. Kazi kubwa inayotakiwa ni kutunza miundombinu yote inayojengwa, aliongeza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.