UBORESHAJI wa Miundombinu ya elimu unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umekuwa chachu ya ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali Jiji la Dodoma kutoka asilimia 98 hadi 115 kwa mwaka 2024.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipokuwa akiongelea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa miaka mitatu ofisini kwake.
“Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma tunampongeza sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu na kutujengea shule mpya kupitia mradi wa BOOST na EP4R, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kujengewa madarasa mapya na kuboreshewa miundombinu hali iliyopelekea wazazi na jamii kuona fursa ya kuwaleta watoto wao kupata elimu. Serikali imejitahidi sana kuhakikisha inasogeza huduma ya shule katika maeneo ya wananchi, sasa hivi kwenye kata nyingi watoto wanapata elimu karibu na maeneo wanayoishi ile dhana yakutomuandikisha mtoto shule kutokana na umbali imeisha na shule nyingi zilizokuwepo zimeboreshwa hivyo, kutengeneza mazingira rafiki ya kujifunza.
Akiongelea mafanikio ya Elimu katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita Mwl. Myalla alisema kuwa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma inajivunia ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa Darasa la Saba kutoka asilimia 82.2 kwa mwaka 2021 hadi asilimia 93.18 kwa mwaka 2024
Ongezeko la miundombinu ya elimu limeenda sambamba na ufaulu wa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba, Halmashauri kwa sasa ufaulu umeongezeka hadi kufikia asilimia 93.18. Hii ni kutokana na wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri na tulivu, ukilinganisha na miaka iliyopita. Pia serikali imeongeza vifaa vya kufundishia sasa hivi kila mwalimu anatumia vifaa vya TEHAMA hivyo, kuwafanya walimu na wanafunzi kwenda na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Dodoma English Medium, Evodius Kanizio aliishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 458 kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya Mtaala wa kingereza jijini Dodoma. “Shule yetu ni shule ya mchepuo wa kingereza inayomilikiwa na serikali imeanza rasmi mwaka 2024, kwa sasa tuna jumla ya watoto 267 kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu. Ujenzi wa shule hii umegharimu kiasi cha shilingi milioni 458 ambazo kati ya hizo milioni 400,000,000/= zimetolewa na Serikali kuu na Milioni 58,000,000/= zimetolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mapato yake ya ndani. Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi hii ya kutoa elimu bora kwa mtaala wa Kingereza kwa watazania. Hapo awali hatukuwa na shule za mtaala wa kingereza, tulizoea kujenga shule za mtaala wa Kiswahili ila kwa maono ya Rais wetu akaona tunaweza toa elimu bora ya Kingereza kama shule nyingine za binafsi. Shule ambazo zitawafikia wananchi wa kipato cha kati ambao hawawei kumudu gharama za shule binafsi kupata elimu kwa gharama nafuu” alisema Kanizio.
Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma ina jumla ya shule 176 ambazo kati ya hizo 104 ni za Serikali na 72 ni za watu binafsi, ina wanafunzi 138,679 pia ina idadi ya walimu 1862.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.