Na. Aisha Ibrahim, UHURU
Diwani wa Kata ya Uhuru, Halfan Kabwe, ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa ya kukuza sekta ya elimu kwa maendeleo ya Jiji la Dodoma na taifa kwa ujumla.
Alitoa shukrani hizo wakati akitoa ufafanuzi wa pesa alizopokea katika kata yake kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Uhuru, uliogharimu shilingi milioni 76.
Akitoa ufafanuzi wa kina kuhusu ukamilifu wa vyumba vya madarasa alisema, “kupitia serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitupatia kiasi cha shilingi milioni 50 ambazo tuliweza kujenga madarasa 10 na baadae akatuongeza kiasi cha shilingi milioni 26 zilizotuwezesha kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo” alisema Diwani Kabwe.
Katika hatua nyingine, alimpongeza mbunge kwa kuwa na moyo wa kujitolea kufuatia ujenzi wa uzio katika shule hiyo kwalengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kupitia mazingira rafiki. “Nichukue fursa hii kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, kwa kutusaidia kujenga uzio wa shule hii kwa kutumia fedha zake mwenyewe ambapo kabla ya hapo kulikuwa na changamoto kwa wanafunzi kwasababu sehemu kubwa ya shule hii ilikuwa imevamiwa na magari ya mizigo” alisema.
Pia, aliahidi kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu ikiwemo kutunza miundombinu ya shule hiyo na kupandisha ufaulu wa wanafunzi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla. “Tunaahidi kufanya makubwa katika sekta ya elimu ikiwemo kutunza miundombinu ya shule hii na kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa kiwango cha juu kwasababu Dkt. Samia Suluhu Hassan anatudai deni kubwa sana kupitia uwekezaji huu” aliongeza Diwani Kabwe.
Kwa upande wake, Mwl. Sospeter Ramadhan, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, alieleza kuwa kabla ya kujengwa kwa uzio wa shule hiyo kulikuwa na changamoto kwa wanafunzi katika suala ya nidhamu na taaluma. Sababu kubwa mazingira hayo yamezungukwa na wafanyabiashara wengi waliokuwa wanasababisha muingiliano na wanafunzi jambo linalopelekea washindwe kujifunza kwa utulivu.
Sambamba na hayo, mwanafunzi kutoka shule ya Msingi Uhuru, Fathiya Saleh, alieleza kuwa kabla ya kujengwa uzio walikuwa wanakutana na vishawishi mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo hilo. Pia vitisho kutoka kwa walevi na vichaa wanaoingia eneo la shule jambo lililokuwa linapelekea kukosa amani wawapo shuleni hasa kipindi cha mapumziko.
Nae, Ikram Mohamed, mwanafunzi kutoka shule hiyo, aliishukuru serikali kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na uzio kwasababu kabla ya hapo walikuwa wanashindwa kukaa darasani na kusoma kwa utulivu. Pia aliahidi kusoma kwa bidii ili kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.