Wakuu wa Shule, Watendaji wa Kata na Maafisa Elimu, wametakiwa kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa Madarasa na Mahabara katika shule zao, kabla ya tarehe ya kufungua shule kwa muhula wa masomo wa mwaka 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alipokua akizungumza na Wakuu wa Shule, Watendaji Kata na Maafisa Elimu Kata kwenye kikao kazi cha ndani cha kiutendaji kilichokua na lengo la kufanya tathmini ya ujenzi wa madarasa na mahabara katika Shule za Msingi na Sekondari Jijini Dodoma.
Kunambi amesema kuwa iwapo mpaka kufikia tarehe ya kufungua shule ujenzi huo utakua haujakamilika na pesa za kujengea zipo kwenye akaunti na zimeingizwa kwa muda mrefu, viongozi hao waandae maelezo ya kwanini waendelee kuwa katika nafasi walizo nazo.
Vilevile amewataka wakuu wa Shule kuhakikisha wanafunzi wote wanaingia madarasani na kuwafuatilia wale wote ambao hawaingii madarasani, kujua sababu zinazowapelekea kutofanya hivyo.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Idara ya Mipango , Takwimu na Ufuatiliaji wa Jiji la Dodoma Shabani Juma ameshangazwa na baadhi ya wakuu wa Shule jijini hapa, kushindwa kufanya ukarabati mdogo wa baadhi ya vitu katika shule zao kama vile viti, meza na milango licha ya mambo hayo kuwa ndani ya uwezo wao.
Shabani amewataka waalimu hao kutoishi kama wapangaji, huku akiwahimiza kuwa wabunifu na kuzipenda shule zao kutokana na baadhi ya shule kuwa na miradi inayowaingizia pesa ambazo zingewawezesha kukarabati vitu mbalimbali kama vile madawati na milango.
Nae Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Jiji la Dodoma Alfred Mlowe amewakumbusha viongozi hao kuwa fedha zinazotumika katika ujenzi na ukarabati ni fedha za Serikali hivyo matumizi ya fedha hizo yanatakiwa yazingatie na yafuate sheria, kanuni na miongozo ya Serikali kwa sababu mwisho matumizi hayo ni lazima yakaguliwe.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alipokuwa akiongea na waalimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, watendaji na maafisa elimu kata (hawapo pichani) kuhimiza juu ya umaliziaji wa miundombinu ya shule za jiji kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza.
Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji Shabani Juma akiongea wakati wa kikao kazi na watendaji na maafisa elimu kata pamoja na walilmu wakuu wa shule za Jiji la Dodoma.
Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Jiji la Dodoma Alfred Mlowe akizungumza na washiriki wa kikao kazi kilichohusu umaliziaji wa miundombinu ya shule kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.