WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya shule, ikamilike mapema. Amesema kama kuna watendaji walioko likizo warudi, kwani serikali inataka wanafunzi wote waanze masomo pamoja.
Ameyasema hayo juzi wakati alipokagua ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleoa wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Alisisitiza ukamilishwaji wa miradi hiyo ili wananchi waanze kuitumia.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari, Waziri Mkuu alisema agizo alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Desemba 29, 2019 kuhusu usimamizi wa miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa, liko pale pale kwa sababu serikali haitaki kuona wanafunzi wakipishana katika kuanza masomo.
Miradi aliyoitembelea ni ujenzi wa Shule ya Msingi ya Ng’au ambayo ipo hatua za mwisho kukamilika, ujenzi wa chuo cha VETA, Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na Shule ya Sekondari ya Lucas Maria.
Waziri Mkuu alisema serikali inatoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima viongozi katika maeneo husika wahakikishe wanashirikiana katika kusimamia utekelezaji wake.
Alisema wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo mwanzoni mwa mwezi huu, hivyo ni lazima usimamizi ukaongezwa katika baadhi ya maeneo ambayo miundombinu yake haijakamilika ili kuwahi masomo.
Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Lucas Maria, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue ahakikishe mafundi wanafanya kazi usiku na mchana.
“Shule zinakaribia kufunguliwa na baadhi ya majengo kama bwalo, maabara, nyumba za walimu hayajakamilika, mafundi hawapo eneo la ujenzi na Serikali imetoa fedha. Nataka kazi hii ikamilike mapema kwani hakuna sababu,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Wananchi wa wilaya ya Ruangwa wamepongeza na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kutokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Wananchi hao wakiwemo vijana wanaojenga chuo cha VETA, walitoa pongezi na shukrani hizo mbele ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza kukagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho. Mafunzo yatakayotolewa chuoni hapo ni ufundi uashi, useremala, ufundi magari, ushonaji nguo na TEHAMA.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maabara katika Shule ya Lucas Maria, alipotembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya wilaya yaRuangwa, Desemba 31, 2019.
Chanzo: habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.