Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI
Mjasiriamali mwenye ulemavu Bw. Mwita Marwa Maki, mkazi wa jiji la Dodoma ameishukuru Serikali kwa kumpatia mkopo wa asilimia 10 wa kiasi cha shilingi milioni 10 ambao ameutumia kuendeleza kazi yake ya ubunifu wa kutengeneza vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ambavyo vinamuingizia kipato cha kuendesha maisha yake.
Bw. Maki ametoa shukrani zake kwa Serikali, wakati akizungumza na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpanga alipolitembelea banda la Ofisi ya Rais-TAMISEMI kabla ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kuanzia tarehe 11 hadi 13 julai, 2025.
"Najivunia mafanikio yangu yaliyotokana na msaada wa Serikali, nimepata mafunzo ya ufundi chuma (welding) ya miaka miwili katika Chuo cha watu wenye Ulemavu Yombo jijini Dar es Salaam,” Bw. Maki amesisitiza.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amesema Bw. Mwita Maki ni mfano mzuri wa kuigwa kwa wale wanaodhani ulemavu ni kikwazo cha kujikwamua kiuchumi kwani amedhihirisha namna mtu mwenye ulemavu anavyoweza kuboresha uchumi wake na kuwasaidia walemavu wengine kupata vifaa saidizi kama baiskeli za miguu mitatu.
Awali akiwasilisha mafanikio ya uwekezaji, usimamizi na uratibu wa huduma za afya msingi, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amesema Bw. Mwita Maki ni mlemavu aliyenufaika na mkopo wa Asilimia 10 ambao umemuwezesha kuwa na karakana inayotengeneza baiskeli za miguu mitatu ambazo anaziuza kwa kila moja kwa kiasi kisichozidi shilingi milioni 1.5
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.