MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amewataka viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutobweteka baada ya kupata hati safi kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa unaoishia Juni 2018.
Akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Jiji Juni 12, Mwaka huu, Kunambi alisema kuwa Halmashauri ya Jiji hilo imefanikiwa kupata hati safi kutokana na kujibu ipasavyo hoja zote 54 zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 na kwamba kati ya hoja hizo, 17 ni hoja za zamani na 37 ni hoja mpya.
“Kutokana na utendaji bora, usimamizi mzuri wa miradi, ukusanyaji mapato kwenye vyanzo vyetu vya ndani, Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumeweza kujibu Hoja zote 54 ndani ya siku 21 kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, tumeweza kupunguza hoja za mkaguzi kwa kiwango cha hoja 77, ukilinganisha na hoja za mwaka wa fedha 2016/17 ambapo tulikuwa na jumla ya hoja 131” Alisema Kunambi.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, kutokana na watendaji bora wa Halmashauri yake pamoja na madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano katika suala zima la kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa kiwango kikubwa ndiyo sababu ya kuweza kupunguza hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kila mwaka.
‘’Nawapongeza watendaji wa Halmashauri na madiwani kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kufanikiwa kupata hati safi, hivyo nawaomba muongeze kasi zaidi kiutendaji na kamwe msibweteke,’’alisema Kunambi
Hata hivyo, Katika ukaguzi wa fedha wa mwaka 2017/18 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali ametoa hati safi yenye msisitizo, na kwa upande wa mifuko mbalimbali, Mdhibiti ametoa hati safi kwa mifuko yote kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Aidha, Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Devis Mwamfupe amesema kuwa kupatikana kwa hati safi katika Halmashauri hiyo kutachochea zaidi kasi ya utendaji kazi ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mwamfupe aliwahimiza Madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuwataka kuwatendea haki wananchi ambao wamewachagua kwa kuhakikisha maendeleo yanawafikia kwa kuwatataulia kero zinazowakabili.
Kwa upande wa Mkaguzi Mkuu wa nje wa Mkoa wa Dodoma Chami Ngelela amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa mwaka wa pili mfululizo na kuendelea kuitetea hati hiyo na kupongeza ushirikiano mzuri wanaopatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuweza kujibu hoja zinazotolewa kwa wakati.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.