RAIS Dkt. John Pombe Magufuli jana ameongoza waombolezaji kuaga kitaifa mwili wa Rais wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa huku akisema kiongozi huyo alikuwa shujaa wake na mtu muhimu katika historia ya maisha yake.
Shughuli hiyo ya kuaga kitaifa ilifanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako maelfu ya waombolezaji wakiwamo viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walijitokeza.
Mkapa ambaye aliongoza nchi kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, alifikwa na mauti kwa mshtuko wa moyo Alhamisi ya Julai 23, mwaka huu katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli akihutubia taifa katika shughuli hiyo, mara kadhaa alikuwa akitulia na kutokwa machozi hadharani, hasa alipoanza kuelezea mazungumzo yake ya mwisho na Mkapa.
“Nilipata fursa ya kuongea na mzee Mkapa kwa simu akiwa hospitalini saa chache kabla hajafariki, nakumbuka aliniambia John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri, sikujua kwamba maneno yale yalikuwa ya kuniaga, kazi ameikamilisha. Namshukuru Mungu kwa zawadi ya Mkapa,” alisema Rais Magufuli huku akitoa kitambaa kufuta machozi.
Alisema hakuna mtu anayeweza kumwelezea vizuri Mkapa zaidi ya alivyojieleza mwenyewe kwenye kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’. (Maisha Yangu, Dhamira Yangu).
“Kama ambavyo nimekuwa nikisema bila Mkapa huenda mimi nisingekuwepo hapa nilipo, ni mtu muhimu katika historia ya maisha yangu.
“Hata nilipopatwa na shida au kupambana na changamoto mbalimbali hakuniacha, hakutaka nianguke.
“Mzee Mkapa alinilea kama mtoto wake, alikuwa ni shujaa wangu, alinionyesha upendo, hata kwenye shida Mzee Mkapa hakuniacha kamwe, hakutaka nianguke, alinilea kama mtoto wake. Wakati wote alikuwa ananionyesha upendo, hivyo basi kuondoka kwake ni pigo kubwa kwangu, nimepoteza mtu muhimu katika maisha yangu.
“Saa nyingine machozi yanakuja tu, msinishangae sana, hata mzee Kikwete (Jakaya Kikwete) nilimuona juzi anadondosha machozi, tena Kikwete ni Kanali lakini alitoa chozi, kwa hiyo msinishangae mimi,” alisema Rais Magufuli.
Vilevile Rais Magufuli alisema kuwa kifo cha Mkapa ni pigo kubwa kwa taifa kwa kuwa ilizoeleka katika matukio mengi ya kitaifa amekuwa akiungana na marais wastaafu; Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.
Aidha alisema Mzee Mkapa alikuwa na vipaji vya kiuongozi vya kulea na kukuza na kwamba hata yeye aliibuliwa na kiongozi huyo.
Pia alisema Mkapa ndiye aliyemwibua Kikwete baada ya kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 na baadaye akawa mrithi wake.
“Yeye alimwibua Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. (Ali Mohamed) Shein baada ya kifo cha Makamu wa Rais, Hayati Omari Ally Juma na alimwibua Dk. Hussein Mwinyi kama mnavyofahamu hivi sasa ni mgombea urais Zanzibar, hii inadhihirisha Mzee Mkapa alikuwa na uono wa kuona viongozi.
“Mzee Mkapa alimwibua Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye kwa sasa ni mgombea urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa mwandishi wake wa hotuba Balozi Ombeni Sefue, baadaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi,” alisema Rais Magufuli.
Kiongozi huyo wa nchi aliwasili mkoani Mtwara jana jioni tayari kwa maziko yatakayofanyika leo katika Kijiji cha Lupaso wilayani Masasi.
Chanzo: mtanzania.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.