Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MWENYEKITI wa Mtaa wa Nzasa katika Kata ya Chihanga, Patrick Chanzi (anayechomwa chanjo pichani) ameongoza wananchi wake kupata chanjo ya ugonjwa wa virusi vya Korona (UVIKO-19) baada ya kupata elimu sahihi juu ya chanjo hiyo.
Chanzi alisema kuwa elimu juu ya chanjo ya UVIKO-19 ni muhimu sana kwa sababu ugonjwa huo unaua na kuacha madhara makubwa katika jamii. “Mimi mwenyewe sikuwa na uelewa kabisa kuhusu chanjo hii. Ila baada ya wataalam kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa elimu hapa, nimeelewa na kuchanja. Nimefanikiwa kuwaita wananchi wangu nao kupata elimu hiyo na nimeongoza zoezi la uchanjaji mbele yao na wao kufuata kwa kuchanja. Niwaombe sana wananchi wa Nzasa kujitokeza na kuchanja kwa hiari” alisema Chanzi.
Akitoa elimu juu ya umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19, Afisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia alisema kuwa chanjo hiyo ni salama. Alisema kuwa awali serikali ilisita kuruhusu chanjo hiyo kutolewa nchini kwa sababu ilikuwa haijaifanyia utafiti na kujiridhisha juu ya usalama wake. “Ndugu zangu, chanjo hii ni salama. Serikali imefanya utafiti kupitia mamlaka zake na kujiridhisha kuwa ni salama ndiyo ikaruhudu ianze kutumika nchini” alisema Mahia.
Chanjo hii ni muhimu kwa sababu inasaidia kuepusha maambuzi ya virusi ya Korona na vifo kwa asilimia kubwa. Alisema kuwa pamoja na wananchi kujitokeza na kuchanja bado taratibu nyingine za kuchukua tahadhari zinatakiwa kufuatwa za kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na kuvaa barakoa sehemu zenye mikusanyiko.
Afisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia akitoa elimu kuhusu chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi wa Mtaa wa Nzasa katika Kata ya Chihanga Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.