Kamati ya siasa Wilaya ya Dodoma imefanya ziara kutembelea miradi ya afya na elimu pamoja na ujenzi wa hoteli itakayomilikiwa na Jiji la Dodoma na kuimwagia sifa ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kusimamia na kutekeleza miradi hiyo ambayo kwa asilimia kubwa imetokana na mapato ya ndani.
Akizungumza wakati wa kufanya majumuisho ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, Elirehema Nassari amepongeza ubora na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ambayo ni shule, zahanati na hoteli huku akisema watanzania wamezoea kuona malumalu zikiwekwa kwenye shule za watu binafsi lakini kwa Jiji la Dodoma wanashuhudia malumalu zikiwekwa katika shule za umma.
Nassari ameongeza kuwa Jiji la Dodoma limekua ni jiji la kimkakati na mapato yake yamekua hayatokani na vyanzo vya kimazoea, mfano soko na maeneo ya kuegesha magari kama ilivyo kwa Halmashauri nyingine walizowahi kutembelea.
“Jiji la Dodoma mnajenga hoteli kubwa itakayoitwa Dodoma city Hoteli, mnajenga eneo la kupaki malori kule Nala, mnajenga maeneo mengi ya kimkakati ambayo kazi yake kubwa ni kuongeza mapato. Mmetuambia baada ya mradi huu kukamilika mwezi wa nane mnatarajia kuvuna zaidi ya bilioni tatu ambayo itakua ni faida kwa wananchi wa Jiji la Dodoma. Hivyo nitoe pongezi sana kwa Mkurugenzi pamoja na Mshahiki Meya wa Jiji la Dodoma kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya” alisema Nassari.
Akiongelea kuhusu changamoto ya madarasa katika Jiji hilo, Mchumi wa Jiji la Dodoma, Shabani Juma amesema kuwa Jiji limejipanga kuhakikisha linatatua kero ya madarasa. “Tayari kuna madarasa zaidi ya 150 ambayo yamekwishajengwa huku ujenzi wa madarasa mengine ukiendelea kwa fedha za mapato ya ndani” alisema Juma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.