Na. Hellen M. Minja
Habari – DODOMA RS
Mkoa wa Dodoma unatarajia kukua kiuchumi kutokana na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita kuwekeza katika Mkoa huu miradi ambayo italeta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya uchumi yatakayoleta chachu ya ukuaji wa Pato la mtu mmoja mmoja ndani ya Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameyasema hayo Septemba 24, 2025 alipokua akifungua kikao chake na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi yake Jijini Dodoma kikijumuisha mawasilisho ya mada mbalimbali.
“Dhamira ya Serikali kuwekeza Dodoma ni kubwa sana na miradi itakayotekelezwa italeta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, matamanio ni kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja kwa kuhakikisha wananchi wanatumia miradi hiyo kuwekeza ili kujiongezea kipato.”
Ameongeza kuwa, miradi ambayo ipo kwenye mpango wa utekelezaji ni upanuzi wa barabara ya Mtumba, Treni ya ndani kwa lengo la kupunguza msogamano wa magari sambamba na ujenzi wa Mabwawa sita ambayo yatapokea maji kutoka Mkoa wa Morogoro ili kuepusha adha ya mafuriko.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amesema Mashirika yasiyo ya Kiserikali yamekua na mchango kwa kuisaidia Serikali kutoaji huduma kwa wananchi katika sehemu ambazo haijazifikia hivyo ametoa wito kwa mashirika hayo kufanya kazi kwa mipaka na kuzingatia Sheria na taratibu.
Kadhalika, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Honorata Rwegasira amesema Mashirika hayo yamesaidia kuleta maendeleo kwa jamii kwa kuboresha hali ya maisha ambapo yametumia takribani shilingi Bilioni 65.9 kutekeleza shughuli mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano.
Mkoa wa Dodoma una Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayotambulika kiusajili 437 ambayo yanatekeleza miradi na shughuli mbalimbali kupitia afua za Elimu, Afya, vikundi vidogo vidogo vya kiuchumi, Mazingira, Haki za binadamiu na usawa wa kijinsia yakiwa na lengo la kuchagiza shughuli za Serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.