Na. Hellen M. Minja,
Habari - DODOMA RS
Ikiwa ni siku ya tatu ya mafunzo kwa Wataalam wanaotoa huduma kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu, leo Januari 17, 2025, Mkoa wa Dodoma umekamilisha mafunzo hayo kwa Halmashauri za Kondoa Mji na Kondoa Vijijini ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Kondoa Irangi, Halmashauri ya Kondoa wa Mji.
Mafunzo hayo yanalenga kukuza uelewa kuhusu namna ya kufanikisha mpango wa kuibua wagonjwa wenye vimelea vya Kifua Kikuu unaotarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi siku ya Jumatatu, Januari 20 kwenye Halmashauri 76 za Mikoa 9 Nchini ambapo Mpango huo mahsusi ulizinduliwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama mnamo Januari 06 Mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yanayoratibiwa na Serikali ya Mkoa chini ya Wizara ya Afya, Mratibu wa huduma za kudhibiti Kifua Kikuu kutoka Wizara hiyo Dkt. Allan Tarimo, amesema Mkoa wa Dodoma ndio nyenzo kuu Kati ya Mikoa 9 iliyopo kwenye Mpango kwani ndio Makao Makuu ya Nchi hivyo inabidi kuchimba zaidi ili kuwapata wagonjwa wote.
Aidha, Mratibu wa Huduma za Kifua Kikuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Peres Lukango, amesema;
"Kondoa ina takribani wagonjwa 800 ambao hawakufikiwa mwaka jana hivyo wanatakiwa kuibuliwa wakati wa Mpango huu na tukiwa na dhamira moja, tutaweza. Leo tunamalizia mafunzo kwa Halmashauri zote 7 zilizopo kwenye Mpango, Wataalam wamendaliwa vizuri vituoni na nyenzo zote zimekamilika tayari kwa kuanza zoezi."
Kadhalika, Mshauri wa zoezi la kuibua wagonjwa wenye vimelea vya Kifua Kikuu kutoka Wizara ya Afya nchini Uganda Dr. Turyah Stavia, amehudhuria mafunzo hayo ili kutoa uzoefu wa nchi yake ambayo imefanikiwa kwenye zoezi hilo.
"Nimekuja kutoa msaada kwa Wizara ya Afya kwenye hii kampeni kwa kuwa ukitafuta wagonjwa wa Kifua Kikuu, utawapata. Tunahitaji kumaliza Kifua Kikuu ifikapo 2030 na hatuwezi bila kuwapata wagonjwa wote. Tunapaswa tujiulize nini cha kufanya ili wapatikane? Na ndio kinachofanyika hapa." Dr. Stavia.
Mkoa wa Dodoma unatarajia kuibua wagonjwa wenye vimelea vya Kifua Kikuu wapatao 1,930 ambao hawakupatikana wakati wa zoezi la mwaka 2024.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.