KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za mitaa (USEMI) ikiongozwa na Jaffari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala haijaridhishwa na kasi ya Ujenzi wa Shule mpya maalum ya Sekondari ya Bweni na sayansi ya Wasichana katika Mkoa Kagera kupitia Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Hayo yamebainishwa leo tarehe 25 Oktoba, 2022 wakati Kamati hiyo ya USEMI ikipokea na kujadili taarifa kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya 10 za wasichana zinazojengwa katika mikoa 10 ya awali ambapo kila mkoa utajengewa shule moja.
"Leo tumepokea taarifa za ujenzi wa shule mpya katika mikoa 10, Wapo waliofikia asilimia 80 lakini Kamati imesikitishwa sana na Mkoa Kagera, ujenzi unaenda taratibu mno na bado wapo chini ya asilimia ambayo tuliitarajia”, amesema Chaurembo
Kamati ya USEMI imeuagiza Uongozi wa Mkoa Kagera kuhakikisha wanasimamia mradi wa Ujenzi wa shule hiyo uende kwa kasi inayotakiwa ili ifikapo tarehe 31 Disemba, 2022 ujenzi uwe umekamilika kwa ajili ya kupokea wanafunzi Mwezi Januari 2023.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya USEMI, Chaurembo amepongeza hatua za ujenzi zilizofikiwa katika mikoa 9 na ameutaka Mkoa Kagera ndani ya siku mbili kuwasilisha mpango kazi kwa kamati wa namna watakavyoweza kukamilisha Ujenzi Shule hiyo kwa Wakati.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Angellah Kairuki amesema Serikali ilitoa Bilioni 3 kwa kila mkoa katika Mikoa 10 na ikaagiza kufikia tarehe 31 Disemba, 2022 Ujenzi wa madarasa na miundombinu yote iwe imekamilika kwa viwango kulingana na miongozo iliyowekwa.
Waziri Kairuki amesema Wizara itahakikisha inaweka kambi katika Mkoa wa Kagera na Mwanza na mikoa mingine ambayo ipo nyuma katika utekelezaji wa Miradi hiyo na akaitaka Mikoa yote ihakikishe inajiwekea mpango kazi ya kukamilisha Ujenzi wa Shule hizo wakati taratibu za usajili zinaendelea.
Vile vile, ametoa wito kwa Mikoa mingine kuanza maandalizi ya Ujenzi wa Shule Mpya za wasichana zitakazojengwa kwa mikoa yote nchini kwa awamu ili kuondokana migongano.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.