Mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam na timu ya Taifa Tanzania, Ali Mayai Tembele jana amewapa semina wachezaji na viongozi wa timu ya mpira wa miguu ya Dodoma Jiji FC, ili kuleta uelewa mpana kwa wachezaji na viongozi katika kuwajengea uwezo wa kujitambua na kutimiza majukumu yao.
Semina hiyo, iliandaliwa na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mayai, amesema kuwa historia haitengenezwi na mtu aliyepoteza na washindi ndio huandika historia. Amesema kuwa ukipata fursa ya kucheza kwenye timu na viongozi wana timiza majukumu yao, kilichobaki ni kutimiza wajibu na kufikia malengo.
“Wachezaji wanajua kucheza mpira lakini kuujua mpira ni kitu ambacho hukipati uwanjani, ndani utafundishwa kucheza mpira lakini kuujua mpira, tasnia ya mpira ni zaidi ya kucheza mpira ni pamoja na maisha ambayo mchezaji unatakiwa kuishi” ameongeza Mayai.
Nae, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shabani Juma, ambaye ni katibu wa kamati ya uongozi wa timu ya Dodoma Jiji FC, ameonesha kuvutiwa na semina na kutaka kuwe na muendelezo katika kuzungumza na wachezaji katika kuwajenga ndani na nje ya uwanja.
“Lengo ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili waweze kucheza mpira wa kisasa, kwa sababu kuna mafundisho ya uwanjani na mafundisho ya nje ya uwanja ambapo wachezaji wengi wa kitanzania wamekuwa wakiyakosa, kwahiyo, sisi Dodoma Jiji tumeanza, hii ni hatua ya awali lakini kuna muendelezo ili kuwatengeneza watumishi lazima uwafanyie semina” amesema Juma.
Kwa upande wake, Kapteni wa timu ya Dodoma Jiji, Mbwana Kibacha ametoa shukrani kwa mkufunzi kwa semina na kuongeza kuwa elimu waliyonayo haitoshi ila kupitia semina inawaongezea uelewa katika maisha ya ndani na nje ya uwanja na kuwaonesha njia sahihi katika maisha kwa ujumla.
Wachezaji wa timu ya Dodoma Jiji FC wakiwa na usikuvu mkubwa wakati semina ikiendelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.