Na. Theresia Nkwanga, DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wanufaika wa mkopo wa asilimia 10 ya Halmshauri kuhakikisha wanarejesha fedha za mikopo kama sheria inavyowataka ili fedha hizo ziweze kuwanufaisha watanzania wengine wanaohitaji mkopo.
Wito huo ameutoa aliposhiriki tukio la utoaji Hundi ya mfano kwa vikundi vilivyopata mkopo vya wanawake, vijana na wenye ulemavu tukio lililofanyika katika bustani ya mapumziko ya Chinangali iliyopo jijini Dodoma.
Senyamulle alisema kuwa ni wakati sasa kuhakikisha wanufaika wa mkopo wanatumia mikopo waliyopewa na Halmashauri kimkamkati, kiufanisi na kwa umakini mkubwa kwenye kujikomboa kiuchumi na kurejesha kwa wakati ili watanzania wengine waweze kufaidika.
“Matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kwamba mkikopeshwa fedha hizi mtazirejesha ili na wenzenu waweze kukopa, ningetamani kuona kila aliyepewa fedha hizi anaziheshimu, fedha hii sio zawadi ni fedha ya mkopo na dawa ya mkopo ni kulipa. Nitoe wito kwenu twende tukapeane shime, tukashikamane tukanyoosheane vidole fedha hizi tuzirudishe ili na wenzetu wapate bahati tulopata sisi na sisi tupate bahati yakukopeshwa tena kiasi kikubwa zaidi yatulichopata leo.
Nikuagize Mkurugenzi sheria inaruhusu mtu ambaye hajarudisha mkopo kushtakiwa mahakamani na kufunguliwa kesi, Hili limekua likifanyika kwa uzembe kidogo na kwa huruma sana, ni wakati sasa tuamue kukaza kidogo ili wajue kuwa fedha hii si yakuchezea pia tutawafundisha matumizi ya fedha yanataka nidhamu’’.
Akiongelea dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan, Senyamule alisema dhamira ya Rais Samia nikuhakikisha watanzania wasio na vigezo na wasio na uwezo wa kukopa benki kwenye masharti ya kurudisha riba kubwa na masharti makubwa yakuweka dhamana, wanapata nafasi ya kufanya biashara mbalimbali kwa kukopeshwa na Halmashauri zao mikopo isiyo na riba yenye masharti nafuu yakurejesha ulichokopa tu.
Akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema katika kipindi cha Julai hadi Septemba Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepokea maombi kutoka vikundi 198 vya wanawake vijana na wenye ulemavu yenye thamani ya shilingi bilioni 5.8, baada ya uchambuzi yakinifu jumla vikundi 102 viliidhinishwa nakupewa mikopo yenye thamani ya sh bil 1.3 kati ya vikundi hivo wanawake ni vikundi 46 vijana 33 na watu wenye ulemavu 23.
Naye, Asha Hamisi Mwenyekiti wa kikundi cha Paza Sauti kilichopo Changombe jijini Dodoma kikundi kinachojishughulisha na kukamua alizeti na kuuza mafuta, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yakuhakikisha watanzania wanafaidika na fedha zao kupitia mikopo isiyo na riba.
“Kwaniaba ya kikundi cha Paza Sauti nimshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kutupatia kiasi cha shilingi milioni tano, kupitia mkopo huu pato letu litaongezeka na mtaji wetu wa biashara unaenda kukua, tumejipanga kurejesha vizuri ili tuweze kupata kiasi kikubwa zaidi awamu ijayo tunawashauri watu walioko mtaani wajitokeze kuomba mikopo hii ni halisi’’.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.