UTEKELEZAJI wa miradi ya kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma umefikia asilimia 85 wakati ikitarajiwa kukamilika na kukabidhiwa tarehe 15 Februari, 2020.
Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa miradi ya kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhandisi Emmanuel Manyanga alipokuwa akitoa maelezo ya miradi hiyo kwa timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wanaotembelea Jiji hilo.
Mhandisi Manyanga amesema “sasa tupo kwenye hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma, Soko Kuu la Ndugai na uboreshaji wa bustani ya kupumzikia Chinangali. Kwa ujumla miradi hii ipo katika furushi moja na inatekelezwa na Mkandarasi Mohammedi Builders Limited. Tupo asilimia 85, na tunatarajia kwa mujibu wa mkataba na makubaliano na Mkandarasi tarehe 15 Februari, 2020 miradi hiyo itakuwa imekamilika na kukabidhiwa.
“Tumeona stendi ni kubwa ikiwa na uwezo wa kuchukua mabasi 100 kwa wakati mmoja. Kuna sehemu za kusubiria abiria kubwa nne ambazo zinauwezo wa kuchukua abiria 1,200 wakiwa wamekaa kwa wakati mmoja” alisema Mhandisi Manyanga.
“Tunaamini matokeo chanya yanakwenda kuonekana katika miradi hii. Wananchi watafurahia utekelezaji wa miradi hii. Miradi hii italeta tija katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kukuza uchumi kwa ujumla” aliongeza Mhandisi Manyanga.
Mratibu huyo alisema kuwa “kazi kubwa ni kuitunza miradi hii. Tutashirikiana na wenzetu wa TARURA katika kutunza miradi hii na kuhakikisha inadumu na kutoa huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu wa Dodoma na wageni”.
Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi ukiendelea na kutarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.