MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amefanya ziara ya nyumba kwa nyumba kutembelea maeneo yenye migogoro ya ardhi katika Kata ya Ipagala ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Kunambi amechukua hatua hiyo baada ya kugundua kuwa, idadi kubwa ya wananchi wanaofika katika Ofisi za Jiji hilo kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali zinazohusu ardhi wanatoka katika Kata hiyo.
Ziara ya Mkurugenzi huyo ililenga kukagua uvamizi wa baadhi ya maeneo uliofanywa na wananchi ikiwemo shule, vituo vya afya, viwanja vya michezo, maeneo ya wazi na hifadhi za barabara.
“Hatuwezi kukubali tukose maeneo ya zahanati, shule, au viwanja vya michezo kwa sababu ya baadhi ya watu wachache wasio waaminifu ambao wamekuwa wakimega na kuuza maeneo ya wazi” Alisema Kunambi.
“Sasa tutengeneze utaratibu wetu kwenye mitaa wa kujisimamia wenyewe katika udhibiti wa mambo yanayokwenda kinyume na utaratibu, viongozi wa mitaa kwa kushirikiana na wananchi wakemee uvutaji wa bangi na madawa ya kulevya kwa watoto, kudhibiti ujenzi holela, na kuwachukulia hatua wanaojenga kwenye hifadhi za barabara” Aliongeza Kunambi.
Naye Diwani wa Kata ya Ipagala Kamuli Gombo alisema kuwa, kwa muda wa miaka 26 sasa wananchi wamepimiwa eneo hili lakini migogoro haijawahi kuisha kwa sababu ya kuendekeza urafiki kati ya viongozi na wananchi.
“Kama kuna mtu anastahili kubaki na abaki, lakini kama kuna mtu hastahili na atoke ili suala hili liishe” Alisema Gombo
Baadhi ya Wananchi wamempongeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kutembea nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa kwa kuwa kitendo hicho kimelenga kutatua migogoro yao iliyodumu kwa miaka mingi.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma yupo katika ziara ya mtaa kwa mtaa kwenye Kata zote zenye historia ya migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu kwa lengo la kumaliza kero hizo ili wananchi waendelee kujenga na kuendeleza makazi yaliyopangwa ndani ya Jiji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.