Uongozi wa timu ya mpira wa miguu ya Dodoma FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, umeshauriwa kutumia vyombo vya habari kuitangaza timu hiyo na kuhamasisha wananchi kuiunga mkono.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Msaidizi-Huduma za Habari na Picha wa Idara ya Habari-MAELEZO, kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Rodney Thadeus ofisini kwake leo, alipokuwa akiongelea umuhimu wa vyombo vya habari katika kuitangaza timu ya Dodoma FC.
Rodney alisema kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuitangaza timu hiyo kwa wananchi na kuushauri uongozi wa timu hiyo kutumia vyombo mbalimbali vya habari kama redio, magazeti na mitandao ya kijamii kuhamasisha wananchi wa Dodoma.
“Watu wanataka kupata taarifa kuhusu timu yao kila mara ili wahamasike katika kuisaidia na kuishangilia pale inapokuwa na mechi. Sasa hili ni jukumu la Afisa Habari wa timu. Karibu Redio zote zina vipindi vya michezo, hivyo tengenezeni mtandao utakaowasaidia kuitangaza timu ya Dodoma FC kupitia vipindi hivyo”, alisema Rodney.
Mkurugenzi huyo Msaidizi alisema kuwa mafanikio ya timu yanategemea sana hamasa kutoka kwa wachezaji wenyewe na mashabiki wa timu hiyo na ili kufanikisha hilo, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi timu hiyo inapocheza ili kuwapa hamasa wachezaji. “Mimi nimeishajiwekea utaratibu pale ambapo sina majukumu ya kikazi, mechi zote za Dodoma FC nitakuwa nahudhuria maana hii ndiyo timu yetu wana Dodoma na tunatakiwa tuisaidie ili iweze kupanda ligi kuu. Makao Makuu ya nchi lazima yawe na timu inayoshiriki ligi kuu na timu hiyo ni Dodoma FC ambayo tunatakiwa kuipa hamasa”, alisisitiza Rodney.
Aidha, Rodney aliupongeza uongozi wa Dodoma FC kwa kuitafutia timu hiyo michezo ya kujipima nguvu dhidi ya timu zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara. “Nilishuhudia mechi iliyopita baina ya Dodoma FC na Mbeya City ambapo timu hizo zilitoka sare tasa na leo nasubiri Dodoma FC itakapoivaa Lipuli FC kutoka Mkoa wa Iringa” alisema Rodney.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Dodoma FC, Ramadhani Juma alisema kuwa mchezo wa leo dhidi ya ‘Wanapaluhengo’ Lipuli ya Iringa ni fursa kwa mashabiki na wadau wa Dodoma kwenda kujionea timu yao ikiwa imesukwa upya kwa ajili ya kujiwinda na ligi kuu daraja la kwanza inayotarajia kuanza hivi karibuni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.