MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amewaomba madiwani, watendaji wa kata na wenyeviti wa mitaa kutumia mamlaka walionayo kwa mujibu wa sheria kuhimiza suala la usafi wa mazingira yawe safi na salama ili Makao Makuu ya nchi yawe mfano.
Kauli hiyo ameitoa katika mkutano wa wadau wa taka ngumu kutoka Kata nane za Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Nashera iliyopo jijini Dodoma.
Kunambi amesema kuwa Madiwani, Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Mitaa wanawajibu wa kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao kwa lengo la kuweka mazingira safi. Aidha, aliwataka kuhakikisha Jiji la Dodoma ambalo ndio Makao Makuu ya serikali linakuwa la mfano, na kuongeza kuwa hakuna maendelo yanaweza kuja bila kuwa na afya njema.
“Ndugu zangu nyinyi ndio viongozi ambao mpo karibu na wananchi. Hivyo, nawaomba mtumie mamlaka yenu mlionayo kwa mujibu wa sheria kuwa na ajenda ya usimamizi wa usafi wa mazingira katika mitaa na kata mnazoziongoza. Lengo letu ni kulifanya Jiji letu kuwa la mfano kwa kila kitu, ukusanyaji wa mapato na usafi wa mazingira. Makao Makuu ya serikali lazima yawe safi na salama.
“Mimi naamini kuwa, umoja wetu ndio ushindi wetu, tuna kila sababu Jiji letu liwe na mazingira safi na salama. Tunayo kampuni inayosimamia udhibiti wa taka ngumu ‘Green West’ yenye vifaa vyenye teknolojia ya juu na hivi leo wamekuja na mfumo wa urahisishaji kwa utoaji huduma kwa walengwa kupitia teknolojia ya ‘Tagging system’. Hivyo, tunapaswa kuwaunga mkono ilituweze kufanikisha usafi wa mazingira katika Jiji la Dodoma” alisema Kunambi.
Nae Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti taka ngumu wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro amewaomba wananchi wa Jiji hilo kuunga mkono mfumo huo mpya wa utoaji huduma kwa walengwa kupitia teknolojia ya ‘Tagging system’, ufungwe katika nyumba zao kwa sababu mfumo huo utasaidia sana ukusanyaji wa mapato na taka, hivyo kutatua baadhi ya changamoto walizokuwanazo katika utoaji huduma kwa ukweli na uwazi, jambo litakalosaidia sana kutoa takwimu halisi.
“Ujio wa mfumo huu wa utoaji huduma kwa walengwa kupitia teknolojia ya kisasa ‘tagging system’ utasaidia na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa wakusanyaji taka ngumu na utatusaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizokuwepo hapo awali. Hivyo, nawaomba wananchi wa Jiji la Dodoma kuunga mkono wafungiwe nyumbani kwao teknologia hii ili iweze kulifanya Jiji letu kuwa safi” alisema Kimaro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Green West Pro Limited, Deusgratis Lutazar alisema malengo ya kuweka mfumo huo wa ‘tagging system’ ni kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi wa Jiji la Dodoma. Mfumo huo utatambua idadi ya watu wanao wahudumia katika Kata na Mitaa, alisema. Mfumo utasaidia kuzuia upotevu wa makusanyo ya mapato kutoka kwa wananchi wanaolipia huduma ya kuzolewa taka ngumu nyumbani kwako, alisisitiza.
“Sisi kama kampuni ya Green West Pro Limited tumeamua kuleta mfumo huu mpya wa teknolojia ya ‘tagging system’ ambao utatusaidia katika kutambua wateja wetu kwa ngazi zote za mitaa na kata. Licha ya kutambua, Lakini pia tunatumaini mfumo huu unakuja kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wetu lna pia kutatua changamoto tulizo kuwa tunakabiliana nazo katika kutoa huduma zetu. Tunawaomba wananchi wa Jiji la Dodoma kutuunga mkono katika hili” alisema Lutazar.
Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti taka ngumu wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro akiongea wakati wa kipindi cha majadiliano kuhusu changamoto za usafi wa mazingra na utatuzi wake. Kulia kwa Kimaro ni Mwenyekiti wa Mkutano huo Diwani wa Kata ya Mkonze Mhe. David Bochela.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Green West Pro Limited, Deusgratis Lutazar akizungumza jinsi kampuni yake ilivyojipanga kuhakikisha jiji la Dodoma linakuwa safi muda wote kwa kushirikiana na wadau wa usafi na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Washiriki wa mkutano kuhusu usafi jijini Dodoma wakimsikiliza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma (hayupo pichani).
Afisa TEHAMA wa kampuni ya Green Waste Pro Limited Alex akitoa mada kuhusu mfumo ujulikanao kama 'Tagging System' utakavyokuwa ukifanya kazi ili kurahisisha majukumu wadau wa usafi katika kuliweka jiji la Dodoma kuwa safi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.