Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amewaomba wajumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhudhuria kwenye mechi ya ligi daraja la kwanza inayozikutanisha timu ya Dodoma Jiji FC dhidi ya Boma FC kutoka jijini Mbeya utakaochezwa jumapili katika uwanja wa Jamhuri, ili kuongeza hamasa kwa vijana na wananchi kwa ujumla kushiriki katika michezo.
Kunambi ameyasema hayo kwenye kituo cha maegesho ya malori Nala katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa ya CCM waliokuwa kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 43 ya chama hicho. Ziara hiyo ilihusisha wilaya 7 na kuhitimishia katika Jiji la Dodoma kwa kutembelea miradi ya kimkakati inayojengwa chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi Kunambi alisema vijana walioko katika timu inayomilikiwa na Jiji hilo, Dodoma Jiji FC wanajituma kwa hali na mali katika kuinua soka jijini hapa ambapo timu inashika nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi Daraja la Kwanza nchini.
“Hapa ni kituo cha maegesho ya magari makubwa ya mizigo ikiwa ni awamu ya kwanza ambapo katika ujenzi wa awamu ya pili tumejipanga kuongeza viwanja vya michezo ya mpira wa miguu na mpira wa kikapu, pia hosteli itakayotumika kwa ajili ya vijana wetu wa Dodoma Jiji FC, vyote vitajengwa pembezoni mwa kituo hiki .
“Hadi hivi sasa Dodoma Jiji FC ni kinara wa ligi ya daraja la kwanza, na siku ya jumapili itacheza katika uwanja wa Jamhuri hapa hapa nyumbani, niwaombe Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote mfike ili kuwapa 'sapoti' na kujionea uwezo wa vijana wetu wanaotuwakilisha vyema katika soka,” alisisitiza Kunambi.
Mkurugenzi huyo alisema siyo tu kwenye miradi ya kimkakati bali Halmashauri ya jiji inafanya vyema hata katika upande wa michezo wako vizuri, na malengo yao kwa sasa ni kufanya jitihada zitakazowezesha kuifikisha Dodoma Jiji FC katika ligi kuu ya Tanzania bara.
“Heshima kubwa tuliyopewa na mheshimiwa Rais John Magufuli ya kujenga uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu laki moja kwa wakati mmoja, lazima tuwe na timu ambayo iko ligi kuu.
“Tunakwenda ligi kuu, Dodoma lazima tuwe na timu zaidi ya moja, hivyo tujitokeze kwa wingi uwanjani ili vijana wetu wapate morali ya kufanya vizuri zaidi katika uwanja wetu wa nyumbani,” alikazia MKurugenzi huyo.
Ziara hiyo jijini hapo imefanyika kwa siku mbili na kuongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM, Mheshimiwa Godwin Azaria Mkami wenye kaulimbiu ya T tatu ikiwa ni Tumekagua, Tumejionea na Tumeridhishwa. Mwenyekiti alitoa mapendekezo hayo kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa katika mradi wa kimaendeleo wa ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo Nala.
Kikozi cha timu ya mpira wa miguu ya Dodoma Jiji FC kinachoongoza ligi daraja la kwanza nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.