MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ameipongeza Kampuni ya Chemicotex kwa kuchangia juhudi za halmashauri za kutokomeza daraja ziro kwa shule za sekondari katika matokeo mtihani wa taifa.
Kauli hiyo aliitoa leo ofisini kwake alipokutana na kufanya mazungumzo na Meneja wa Kampuni ya Chemicotex tawi la Dodoma Bi. Alice Joseph.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa halmashauri yake inatumia bajeti kubwa katika utekelezaji mipango ya sekta ya elimu na itaendelea kutumia fedha nyingi ili kuifikisha elimu katika viwango vya juu. Alisema kuwa serikali pekee haitoshi, ushiriki wa wadau ni muhimu sana katika kufanikisha mipango ya elimu.
“Kampuni hii ya Chemicotex ni ya kwanza katika kuchangia program hii. Hivyo, niwaalike wadau wengine kuchangia sekta hii ili kwa pamoja tuisogeze mbele. Dodoma kuna watoto wengi wenye akili sana ila changamoto za kimazingira ndizo zinawakwamisha kuweza kufanya vizuri katika masomo yao” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Akiongelea mchango wa wadau, alisema kuwa wadau wanamchango mkubwa katika kufanikisha mipango ya elimu. “Halmashauri tutapanga siku ili tuweze kukutana na wadau mbalimbali na kuwapa muelekeo na maono ya maendeleo ya halmashauri ili waweze kuchangia sekta ya elimu. Serikali hatutanyamaza, tutaendelea kutoa mchango wetu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza sekta ya elimu” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Akiongelea wanafunzi wanaoacha shule kutokana na sababu mbalimbali, alisema kuwa halmashauri itawatafuta na kuwarudisha shuleni. “Dodoma tuna ‘drop out’ ni lazima tuwatafute na kuwarudisha darasani ili tuwakomboe kielimu na kuwawezesha kuwa na mchango zaidi katika taifa lao” alisema Mkurugenzi Mafuru.
kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya Chemicotex tawi la Dodoma, Alice Joseph alisema kuwa ameona inafaa kwa kampuni hiyo kutoa dawa za meno na miswaki kwa wanafunzi wote walio katika mpango wa tokomeza ziro katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Leo tunawakabidhi dawa za meno na miswaki ili muweze kufika mbali katika juhudi zenu za kutafuta elimu” alisema Alice.
Alisema kuwa kampuni yake inatamani kuona kiwango cha elimu kinapanda katika Jiji la Dodoma. Aliahidi kuendelea kushirikiana na jiji hilo katika kuinua masuala ya elimu.
Akimkaribisha Meneja wa Kampuni ya Chemicotex kukabidhi dawa za meno na miswaki kwa wanafunzi, Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatekeleza mkakati wa kutokomeza ziro katika kidato cha nne. “Tunafuraha leo hii kupokea ugeni toka Kampuni ya Chemicotex tawi la Dodoma. Awali tuliwasilisha mpango wa tokomeza ziro katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na leo wametuitikia na kutuletea vifaa hivi mnavyoviona hapa. Tunawashukuru sana kwa mchango wao” alisema Mwalimu Upendo.