MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amewataka watumishi wa Jiji hilo kushirikiana katika majukumu yao ya kazi kitu ambacho kitasaidia kuleta matokeo mazuri kwa manufaa ya Jiji na Taifa kwa ujumla.
Mafuru aliyasema hayo alipokua anafungua mafunzo ya siku moja ya watumishi wa Halmashauri hiyo Idara ya Maendeleo ya Jamii ya jinsi ya kusajili kaya kwenye Bima ya Taifa ya Matibabu ya CHF Iliyoboreshwa yaliyofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri hiyo.
Aidha Mafuru alimpongeza Mkuu wa Idara hiyo Sharifa Nabalang'anya kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaunganisha watumishi wa idara yake kitu kinachopelekea idara hiyo kuwa miongoni mwa idara zenye mafanikio makubwa katika Halmashauri ya Jiji hilo.
"Nikupongeze sana Mkuu wa Idara na watumishi wako kwa utaratibu mliojiwekea wa kukaa na kujadiliana mambo mbalimbali ya kujenga, kwasababu kwa kukaa pamoja ndipo mtagundua mapungufu yenu na nini mkifanye ili kukabiliana nayo, kwasababu kuwa kiongozi haimaanishi kuwa wewe una akili sana kuliko wengine, kwahiyo ukijifungia hauwezi kugundua wapi unakosea na hautafanikiwa" alisema Mafuru.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya alimshukuru Mkurugenzi kwa ukaribu wake na idara hiyo kwani kila wanapompelekea hoja zao amekua akizishugulia kwa ukaribu zaidi.
Nabalang'anya aliongeza kuwa Idara hiyo ina majukumu makubwa ambayo bila kuwa na ushirikiano hawatafanikiwa hivyo waendelee kushirikiana ili kuhakikisha idara hiyo inafanya vizuri jambo litakalowaletea makufaa kwa mtu mmoja mmoja na Halmashauri kwa ujumla.
Akizungumzia kuhusiana na Bima ya Afya ya Jamii (CHF Iliyoboreshwa) Nabalang'anya alisema, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatilia mkazo kuwa kila mwananchi anatakiwa kuwa na bima hiyo na wao ndiyo wahusika wakubwa wa kuhakikisha wanawafikia na kuwasajili watu wengi zaidi ili kutekeleza azma hiyo ya Serikali.
"Niwakumbushe tu kuwa katika vitu ambavyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima anavipa kipaumbele ni pamoja na hii bima ya CHF hivyo tupambane kuhakikisha kila afisa hapa unajifunza na kuelewa ili ukirudi katika eneo lako la kazi unatoa elimu na kusajili kaya nyingi uwezavyo ili kuendana na azma ya Serikali" aliongeza Nabalang'anya.
Naye Mratibu wa CHF Jiji la Dodoma Patrick Sebiga alisema licha ya Jiji hilo kuongoza katika Mikoa iliyosajili Kaya nyingi lakini bado kiwango cha Kaya ni kidogo ukilinganisha na mpango wa Serikali.
Sebiga alisema kuwa, lengo kuu la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kuwafundisha kusajili Kaya kwa kutumia simu za mkononi ili kuhakikisha Kaya nyingi zinafikiwa kwa wepesi na uharaka.
"Msajili anapokua katika Kata inamrahisishia mwananchi kujisajili bila usumbufu wa kufunga safari kuja Halmashauri kufanya zoezi hilo, kwa kufanya hivyo tutazifikia Kaya nyingi kwa muda mfupi na wananchi watanufaika kwa kupata huduma za Afya kwa gharama nafuu tofauti na usipokuwa na Bima." alisistiza Sebiga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.