MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ameridhishwa na ujenzi wa shule mpya ya msingi Mtube katika jitihada za kuboresha mazingira ya kujifunzia wanafunzi iliyopo jijini hapa.
Mkurugenzi Mafuru alipongeza hatua ya ujenzi iliyofikiwa alipoongoza timu ya Menejimenti ya Halmashauri hiyo jana kukagua na kuona hali halisi ya utekelezaji wake katika Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma.
Mafuru alisema “shule hii imejengwa kwa kiwango cha juu. Shule zote zinazojengwa katika Halmashauri ya Jiji zinatakiwa kuwa katika viwango hivi. Hii inaonesha nia njema ya Halmashauri kuboresha mazingira ya kufundishia kwa wa walimu na kujifunzia kwa wanafunzi”.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa shule hiyo, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shaban Juma alisema kuwa Halmashauri ya Jiji iliamua kujenga shule hiyo kutoka mapato yake ya ndani kwa lengo la kupunguza msonganamo katika shule ya msingi Nkuhungu. “Madarasa 10 yamejengwa katika shule hii, na tutaongeza madarasa mengine manne ili tufikishe jumla ya madarasa 14. Aidha, tutanunua madawati yote kwa ajili ya shule hii” alisema Juma.
Majengo mengine aliyataja kuwa ni jengo moja la utawala na matundu ya vyoo yaliyo katika hatua za ukamilishaji. “Katika shule hii mpya takribani shilingi milioni 370 zimekwishatolewa kwa ajili ya ujenzi huu. Utaratibu wa ujenzi unaotumika ni wa ‘force account’ na shule ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 700” aliongeza Mchumi Juma.
Kwa upande wake, Mweka Hazina wa Jiji la Dodoma, Alfred Mlowe alishauri kuwa utaratibu wa kuandaa hati kwa ajili ya shule hiyo uandaliwe. “Kumekuwa na tabia ya wananchi wa maeneo jirani na shule kuvamia maeneo ya shule na kusababisha shule kushindwa kufanya maendeleo na utanuzi wa miundombinu. Ni vizuri mipaka halisi ya shule hii itakambuliwa na utaratibu wa kupata hati ukaanza mapema ili kuondoa migongano hapo baadae” alisema Mlowe.
Nae James Minja, mkazi wa Kata ya Nkuhungu, jijini hapa alisema kuwa shule ya msingi Mtube itakapoanza mapema Januari itasaidia kuboresha elimu katika kata hiyo na kuwapunguzia adha wanafunzi na kusoma katika mazingira bora.
Shule mpya ya msingi Mtube inatarajiwa kufunguliwa rasmi Januari, 2021.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru (kulia) akimsikiliza Shabani Juma (wa nne kutoka kulia) alipokuwa akielezea kuhusu ujenzi wa shule mpya ya Mtube ambayo inajengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. Wengine pichani ni wajumbe wa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma walipofanya ziara kutembelea miradi ya Jiji la Dodoma.
Baadhi ya madarasa ambayo yamekwishakamilika katika Shule ya Msingi Mtube ambayo ujenzi wake unatumia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.