MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amewataka wananchi wote wenye malalamiko na migogoro ya ardhi katika Mtaa wa Kitelela kujitokeza katika shule ya msingi Kitelela kusikilizwa na kutatuliwa migogoro hiyo katika kipindi cha wiki moja.
Mkurugenzi Mafuru alisema hayo alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wenye maeneo katika Mtaa wa Kitelela uliopo Kata ya Nzuguni jijini katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika shule ya msingi Kitelela mwisho wa wiki.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alifanya mkutano na wananchi na kuagiza halmashauri kwenda kutatua migogoro hiyo. “Nimekuja na wataalam wa Ardhi na Mipango Miji wengi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi hapa Kitelela. Tutasikiliza watu 10 wa kwanza kwa ajili ya kukumbushana zile changamoto za jumla za mradi huu wa Kitelela. Kisha tutasiliza kila mwenye ardhi hapa Kitelela na kutatua lalamiko lake. Zoezi hili kitafanyika kama sensa ya watu inavyofanyika, ni mtu kwa mtu hatutaacha hata mtu mmoja ambaye hajasikilizwa na kutatuliwa mgogoro wake” alisema Mafuru.
Katika kufanikisha zoezi hilo bila kusababisha usumbufu kwa wananchi, aliagiza timu ya wataalam wa Ardhi na Mipang Miji kuweka kambi katika shule ya msingi Kitelela kuanzia tarehe 10-15 Januari, 2022. Alisema kuwa wataalam hao watapokea na kusikiliza kila mgogoro na kuutatua. “Kwa ile migogoro ambayo ni lazima kwenda eneo la kiwanja au shamba tutakwenda eneo hilo na kutatua mgogoro husika” alisema Mafuru.
Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi wote wenye ardhi katika Mtaa wa Kitelela kujitokeza katika siku hizo zilizotengwa maalum kwa ajili ya kutatua migogoro hiyo. “Kwa wale wananchi ambao malalamiko yao ni kuondolewa katika maeneo ya asili yaliyokuwepo na kupelekwa maeneo mengine, warudishwe katika maeneo yao yaliyotambuliwa. Wale wananchi wanaolalamikia kuongezewa maeneo na kutakiwa kilipa gharama kubwa warudishiwe maeneo yao ili walipe gharama halisi” alisema Mafuru.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.