Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma amepongezwa kwa kazi nzuri inayoendelea katika ujenzi wa jengo la kisasa la wazi la wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) likiwahakikishia eneo salama la kufanyia biashara zao.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alipoongoza Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Dodoma na viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya mkoa kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo katika eneo la Bahi road leo.
Mtaka alisema “tunawapongeza sana Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri. Naibu Meya peleka salamu kwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na madiwani kwa kazi nzuri. Mkurugenzi wa Jiji tunakupongeza sana. Mradi huu ni kielelezo kwamba una uwezo mkubwa wa kuongoza katika nafasi yako”.
Alisema kuwa matarajio ya watu ni kuona Machinga wakifanya shughuli zao katika maeneo salama. “Matarajio ya watu siyo kuona vinajengwa vibanda vya muda katika makao makuu ya nchi. Tukimaliza mradi huu halmashauri 184 zitakuja kujifunza hapa” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa eneo hilo lina uwezo wa kuhudumia Machinga 3,000. “Lakini pia kuna uwezekano wa kuongeza Machinga wengine kufikia 5,000. Machinga wote waliotambuliwa watasajiliwa katika mfumo wa kieletroniki ili tuwe na kumbukumbu sahihi” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Mradi wa ujenzi wa soko la wazi la Machinga katika Jiji la Dodoma ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutenga na kuandaa maeneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.