MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amepongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha mawasiliano na utendaji kazi baina ya waheshimiwa madiwani na timu ya menejimenti ya Halmashauri.
Pongezi hizo amezitoa leo katika mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani alipokuwa akifafanua hoja zilizotolewa na madiwani katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa, ameona umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kurahisisha ufanisi wa mawasiliano na utendaji kazi katika vikao. “…tumeona umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Mara ya mwisho nilisoma maswali na hoja 82 hapa mbele, na maswali hayo nilikuwa nayo mimi mwenyewe. Leo hii kila mjumbe ametumiwa maswali na majibu ya hoja katika kishikwambi” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Akiongelea matumizi ya TEHAMA katika ufanisi wa kazi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano, Joseph Fungo alisema kuwa “Vishikwambi vimesaidia kurahisisha utendaji kazi, uendeshaji wa vikao na kukuza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilinunua vishikwambi 100 kwa ajili ya Madiwani na Wataalam wake. Vishikwambi hivyo vimesaidia sana kupunguza matumizi ya shajara katika kutengeneza makabrasha na kupunguza gharama za uendeshaji wa vikao na mawasiliano;
Aidha, matumizi ya vishikwambi yamesaidia kurahisisha utaoji na ugawaji wa taarifa na makabrasha ya vikao kwa wakati na hivyo kuondoa zile gharama za matumizi ya magari na mafuta wakati wa kuyasambazia kwa Waheshimiwa Madiwani”.
Akifafanua zaidi alisema kuwa Madiwani na wataalam wanafurahia matumizi ya vishikwambi hivyo. “Kwa kweli tumeona wengi wao wanafurahia na wameweza kumudu matumizi yake kwa haraka. Hili linajidhihirisha kwa mabadiliko ya uendeshaji wa vikao vya Halmashauri. Sasa vikao vinaendeshwa kwa uwazi zaidi na kwa muda mfupi bila kuathiri ubora wa maamuzi na matokeo yake” alisema Fungo.
Naye Mhe. Aloyce Luhega, Diwani wa Kata ya Nzuguni, amesema kuwa “Wazo la matumizi ya vishikwambi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni zuri kwa sababu vinatusaidia kupata taarifa mapema. Ni muhimu kwa sababu vinatusaidia kutunza kumbukumbu kwa urahisi kuliko tulivyokuwa tukitumia makabrasha. Utakumbuka tulikuwa na makabrasha makubwa kwa kikao kimoja jambo ambalo ilikuwa ni shida kwa ubebaji na uhifadhi wake, na unajua yakishakuwa mengi yanageuka kuwa uchafu;
Mimi nimefurahia matumizi ya vishikwambi na niipongeze sana Halmashauri yetu kwa uamuzi huo”. alimalizia Mhe. Luhega.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.