MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru ametoa wiki moja kuanzia Jumatatu ya tarehe 7 mpaka Ijumaa kwa wakazi wa Kata ya Nzuguni kusajili malalamiko na kero zao zinazohusu ardhi kwenye ofisi ya Mtendaji wa Mtaa wa Nzuguni ‘A’ ili maafisa wa ardhi wazichukue na kuzifanyia kazi.
Mafuru ameyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi kwenye kata ya Nzuguni kwa lengo la kujitambulisha na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.
Alisema kuwa baada ya zoezi la kuorodhesha kero kukamilika, siku ya Ijumaa mchana wataalam wa ardhi kutoka Halmashauri ya Jiji watazichukua ili kuzipitia na ifikapo Jumatatu ya tarehe 14 yeye pamoja na wakuu wa vitengo vinavyohusika na masuala ya ardhi na Mkuu wa Idara hiyo wataweka kambi katika ofisi ya Mtaa huo kwa siku tano ili kuzipitia kero hizo moja baada ya nyingine na kuzitatua.
“Baada ya zoezi la kusajili kero kukamilika, Jumatatu inayofuata nitafunga hema katika ofisi ya mtaa na nitahamisha wakuu wangu wa vitengo wote niliokuja nao hapa na mimi mwenyewe nikiwepo pamoja na mkuu wao wa Idara tutahamia hapo, tutaleta na gari tatu, kwa hiyo tutakua tunaangalia kero moja baada ya nyingine kama ni ya kwenda kuona tunaingia kwenye gari tunaenda kuangalia, tunatatua inaisha tunahamia kwa mtu mwingine” Alisema Mafuru.
Mbali na kero za migogoro ya ardhi wananchi wa kata hiyo pia walimuomba Mkurugenzi Mafuru kutatua kero za maji, umeme na barabara katika baadhi ya maeneo ndani ya kata hiyo.
Akijibu kuhusu kero ya umeme na maji Mafuru alisema, ataongea na wakuu wa Taasisi hizo ili kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana kutatua kero hizo huku akiongeza kuwa kumekuwa na mahusiano mazuri kati yao hivyo kuwatoa hofu wananchi wa maeneo hayo kuwa kero hizo zitapatiwa ufumbuzi.
Akijibu kuhusu kero ya barabara mafuru alisema “tuna mitambo iliyoachwa na CDA, tuna greda tatu na mitambo mingine ambayo tumeona tuifufue ili kurahisisha zoezi la utengenezaji wa barabara kwasababu hapo mwanzo tulikua tunatumia gharama kubwa, wataalamu wetu wapo kazini na niwaambie tu kuwa baada ya wiki tatu mitambo hiyo itakua imepona na tutaanza zoezi hilo”.
Aidha Mafuru amewahakikishia wananchi hao kuwa kero zao zitatatuliwa na kila mmoja atapata haki yake, huku akiwaomba kuwa na imani na ofisi yake kwani wapo kwa ajili ya kuwatumikia.
Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa Mtaa huo alimshukuru Mkurugenzi na maafisa alioambatana nao kwa kuja kuwasikiliza na kuchukua kero zao.
Baadhi ya wakazi wa Nzuguni waliojitokeza kumsikiliza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru (hayupo pichani) katika ziara ya kujitambulisha na kutatua kero za wananchi.
Mkutano wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na wananchi wa Nzuguni.
Baadhi ya wataalam wa Jiji la Dodoma walioambatana na Mkurugenzi wa Jiji wakisikiliza kwa makini wakati mkutano ukiendelea.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru (mwenye kipasa sauti) akiongea na wanachi wa Nzuguni (hawapo pichani) kushoto ni wataalam mbalimbali wa Jiji la Dodoma alioambatana nao.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akifafanua kuhusu changamoto na utatuzi wake kwa wananchi wa Nzuguni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.