IDARA ya Mipango Miji, Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaweka kambi ya siku tano kuanzia tarehe 14 Septemba, 2020 kutatua kero za ardhi kwa wananchi wa Mtaa wa Nzuguni “A” Kata ya Nzuguni kwa lengo la kuharakisha utoaji huduma na utendaji haki kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru (pichani juu) alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa za Nzuguni “A” uliopo Kata ya Nzuguni jijini hapa hivi karibuni.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa Mtaa wa Nzuguni “A” una changamoto kubwa ya ardhi baada ya kupimwa na kurasimishwa. “Ndugu zangu nimekuja hapa kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi katika huu Mtaa wa Nzuguni “A”. Kila siku napokea karibu asilimia 80 ya barua za malalamiko ya ardhi kutoka eneo hili. Uamuzi wangu, nitaleta timu ya wataalam wa Idara ya Mipango Miji na Ardhi waje hapa waweke kambi kufuatilia kila mgogoro na kuutatua. Nitaleta gari tatu hapa, afisa anasikiliza mgogoro anaenda eneo la kiwanja kuona hali halisi na kuja na mapendekezo ya utatuzi wa mgogoro husika” alisema Mafuru. Nataka huduma itolewe kwa wananchi hapahapa ili wasipate usumbufu wa kuifuata huduma hiyo makao makuu, haki itatolewa hapahapa, aliongeza Mafuru.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango Miji, Ardhi na Maliasili, Emelye Chaula alisema kuwa maandalizi ya Idara yake kuweka kambi katika mtaa wa Nzuguni “A” yapo katika hatua nzuri. “Kesho Jumatatu tutaweka kambi eneo hilo kwa siku tano ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkurugenzi wa Jiji. Kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kutatua kero zao. Kambi hiyo itategemea na wingi wa watu. Tumeshajipanga na Afisa Mtendaji kuona namna bora ya kutoa huduma hiyo. Kama idadi ya watu itakuwa kubwa sana hatutasita kuongeza idadi ya siku ya kutoa huduma. Tunataka kila mwananchi atatuliwe kero yake” alisema Chaula.
Winifrida Bani ambaye ni mkazi wa Kata ya Nzuguni alisema kuwa ziara ya Mkurugenzi wa Jiji imewapunguzia kero ya kwenda Halmashauri ya Jiji kufuata huduma ya utatuzi wa migogoro ya ardhi katika kata yao. “Mimi nimempenda Mkurugenzi hasa alipoamua kuleta timu yake ya wataalam kuja Nzuguni kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi. Huyu baba kweli anawajali watu wa chini” alisema Bani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.