Na. Josephina Kayugwa, DODOMA.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, aipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa utekelezaji mkubwa uliofanywa wa ujenzi wa miradi ya kimkakati ikiwemo Soko la wazi la Machinga, yenye lengo la kuongeza mapato ya Halmashauri
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa katika ziara ya kukagua na kutembelea mradi wa Soko la wazi la Machinga, alisema mradi huu utasaidia sana wafanyabiashara wadogowadogo kurasimishwa na kufanya kazi katika mazingira mazuri kitu ambacho kitaiongezea mapato Halmashauri.
“Niwapongeze sana kweli mna utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa mapato kwakweli kazi mliyoifanya ni nzuri, lakini pia tuendelee kuongeza ubunifu zaidi katika miradi mingine ambayo itatufanya tutambulike zaidi na kutufanya tuwe wa mfano na watofauti na wengine,” alisema Senyamule.
Aidha Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa katika Soko la wazi la Machinga huduma muhimu ambazo zilikuwa hazijakamilika zifanyiwe utaratibu wa umaliziaji mapema ili wafanyabiashara wakishahamia kusiwe na mgongano.
“ Kuna sehemu za huduma zinatakiwa zikamilike mapema kwasababu muda umeenda kwahiyo Mkandarasi aongeze kasi ya umaliziaji wa soko ili huduma zianze kutolewa mapema, kituo cha magari ya kubeba abiria kikamilike mapema na kianze kufanya kazi na alama za barabarani ziwekwe,” aliongeza Senyamule.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweli alisema mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kutaka Halmashauri zijisimamie kimapato na kuongeza mapato ya ndani.
“Dodoma ndio Makao Makuu tunataka kuwa na sehemu za ufanyaji wa biashara ili Jiji liwe katika mfumo mzuri lakini pia tumeangalia sehemu nyingine za kuongeza mapato,” alisema Shekimweli.
Alimalizia kwa kusema, “lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sio tu kuwapanga na kuwatengenezea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogowadogo bali nikuweka mandhari ya Jiji kuwa safi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.