Na Sifa Stanley, DODOMA.
MKUU wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari Mawasiliano na Uhusiano, (TEHAMA na Uhusiano) wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo amesema kuwa kitengo hicho kina mchango mkubwa katika kukuza mapato ya Halmashauri kupitia mifumo mbalimbali ya ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki.
Aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano maalum kuhusu kazi za kitengo hicho na umuhimu wake katika utendaji wa Halmashauri kwenye zama hizi zinazoshuhudia maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano, ambapo mahojiano hayo yalifanyika katika ofisi za Halmashauri hiyo zilizopo mtaa wa CDA Jijini humo.
Mkuu huyo wa kitengo alisema kuwa, kitengo cha TEHAMA na Uhusiano kina mchango mkubwa katika kukuza mapato ya Halmashauri ya Jiji hilo kwa sababu malipo yote yanayofanyika hutumia mifumo ya TEHAMA.
“Mapato yote yanayokusanywa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma lazima yapite kwenye mfumo wa TEHAMA, tunatumia mfumo wa Wizara ya Fedha unaotumika kukusanya mapato ya Serikali (GePG), mfumo huo unasaidia kutoa namba ya malipo (control number) kwa ajili ya malipo na pia kuna mfumo ambao vyanzo vyote vya Halmashauri vinakusanywa kupitia mfumo wa Mapato ya ndani (LGRCIS) ambao licha ya kukusanya, umesaidia sana kudhibiti upotevu wa mapato” alisema Fungo.
Akiongelea juu ya namna kitengo kilivyojipanga katika mwaka wa fedha ulioanza Julai 2021 hadi Juni 2022, mkuu huyo alisema kuwa kitengo kimejipanga kufanya maboresho kwenye miundombinu na vifaa vya TEHAMA, ambayo yataendelea kuleta mabadiliko chanya katika halmashauri ya jiji na taifa kwa ujumla.
“Kwa mwaka huu wa fedha tumejipanga kufanya maboresho ya miundombinu, tutafanya maboresho ya vifaa, pia tutaimarisha miundombinu. Mifumo mingi inayotumika hapa haijatengenezwa na jiji, inatoka Wizara yetu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa sehemu kubwa sisi ni kujiimarisha katika uboreshaji miundombinu pamoja na vifaa” alielezea Fungo.
Fungo alisema kuwa tayari katika kuhakikisha kuwa mianya ya upotevu wa mapato inadhibitiwa, Jiji limenunua vifaa vya kielektroniki vya kukusanyia mapato (Point of Sell Machines – POS) 292 ili kila chanzo kiwe inakusanywa bila kama ilivyokusudiwa katika Mpango na Bajeti ya Halmashauri.
Akiongelea kuhusu sehemu ya Habari, alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaongeza vitendea kazi vya kisasa ili kuboresha njia zinazotumika kutoa Habari, maudhui, picha za video na za mnato zihusuzo Halmashauri ya Jiji hususani miradi ya maendeleo na Habari zingine mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa Jiji la Dodoma linamiliki kurasa za mitandao ya kijamii (Instagram, facebook), pia tovuti ya Jiji (www.dodomacc.go.tz), jarida linalotoka kila mwezi na televisheni ya mtandaoni (Dodoma City TV).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.