MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj. Jabir Shekimweri aagiza ujenzi wa Zahanati ya Msembeta kukamilika mapema ili wananchi wa Mtaa wa Msembeta waweze kupata huduma za afya karibu na maeneo yao.
Alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Zahanati hiyo mara baada ya zoezi la kukagua na kupanda miti kwaajili ya kutunza mazingira ya eneo hilo kukamilika.
“Zahanati hii ni muhimu kwenu inaenda kuhudumia zaidi ya kaya 486 ambazo zimekuwa zikitembea zaidi ya kilomita 10 kufata huduma za afya Zahanati ya Chigongwe. Hivyo, inatakiwa muongeze kasi mradi ukamilike mapema. Leo tumepanda miti katika eneo hili naomba miti hii itunzwe, ikikua vyema itatupa kivuli na kuwa sehemu ya kupumzikia. Aidha, nawapongeza viongozi na wananchi kwa kuendelea kutekeleza mradi huu licha ya kuwepo kwa changamoto ya maji katika Kata ya Chigongwe. Niwaombe muendelee kuisimamia zahanati hii kwa moyo hadi pale itakapokamilika” alisema Shekimweri.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Chigongwe, Ashirack Rugarabamu aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwaletea fedha kwaajili ya ukamilishaji wa zahanati hiyo. “Tunaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 93,000,000/= kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa mradi huu ambao utakuwa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Kata ya Chigongwe. Kukamilika kwa mradi huu kutapunguzia akina mama wajawazito adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kujifungua, kusogeza huduma ya kliniki ya mama na mtoto pia kusogeza karibu na jamii matibabu ya magonjwa mbalimbali” alisema Rugarabamu.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mapato yake ya ndani imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki. Pia imekuwa ikiunga mkono juhudi za wananchi kwa kutoa fedha kwaajili ya ukamilishaji wa miradi mbalimbali iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.