Na. Josephine Kayugwa, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema wanafunzi wanahitaji kusaidiwa kipindi cha mitihani kwa kuwa watulivu na kufundishwa uzalendo wakiwa shuleni kwa lengo la kuongeza ufaulu bila udanganyifu wowote.
Aliyasema hayo alipokuwa akizindua kitabu cha mwongozo wa mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi katika ukumbi wa mikutano wa shule ya msingi Mtemi Mzengo iliyopo katika Halmasahuri ya Jiji la Dodoma.
“Kitabu hiki cha mwongozo kitumike katika kuwafundishia wanafunzi, katika kipindi hiki cha mitihani watoto wanahitaji msaanda wenu kama walimu. Mnatakiwa kuwapa ushirikiano kwa kuwaelekeza taratibu na sheria za mitihani, tunataka Halmashuri ya Jiji la Dodoma iwe ya mfano katika suala la ufaulu kwa wanafunzi kiwango cha asilimia 87 kiongezeka zaidi katika matokeo yajayo,” alisema Shekimweri.
Aidha, aliongezea kuwa kila mtu ana wajibu wa kulipa kodi kwaajili ya kujenga miundombinu ya elimu ikiwemo shule bora ili kutoa elimu nzuri kwasababu idadi ya wanafunzi wanaosoma kwa sasa ni kubwa. “Serikali inaboresha madarasa na kununua vifaa vya kufundishia kupitia kodi, kwahiyo tuelimishane wote ili kutekeleza jambo hili,” alisema Shekimweri.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prisca Myalla alisema kupitia mwongozo ambao umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, wana matarajio ya kuongeza ufaulu kwa madarasa yote ya mitihani.
“Katika kuongeza ufaulu kwa wanafunzi, tulianzisha vituo rekebishi kwaajili ya kuwasaidia kielimu kwa kuwaelekeza vitu vya muhimu na vyakuzingatia katika masomo na mitihani yao,” alisema Myalla.
Nae Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mtemi Mazengo, Imani Weston alisema kuwa mkakati wa ufundishaji wa kuinua elimu ya msingi utasaidia ili kuweza kunyanyua kiwango cha elimu na kuwasaidia walimu katika ufundishaji.
“Ni kweli kama sisi walimu wakuu, waratibu elimu kata, maafisa elimu wa wilaya na walimu wenzetu kama wataitekeleza mikakati hii kwa sababui imefanyiwa utafiti wa kutosha ninaamini kabisa kiwango cha ufaulu katika shule zetu, kiwango cha ufaulu katika halmashauri yetu na taifa kwa ujumla kitapanda. Ufaulu utaongezeka sana kwa sababu mikakati imelenga changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua ili kuinua kiwango cha elimu katika nchi yetu” alisema Weston.
Ikumbukwe kuwa kitabu cha mwongozo wa mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi ulizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ufunguzi wa mashindano ya michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na mashindano ya michezo katika shule za sekondari (UMISSETA) Mkoani Tabora tarehe 4 Agosti, 2022.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.