Na WJJWM,Arusha.
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amewataka wadau kukabiliana na changamoto ya watoto kupata ujauzito wakiwa wangali shuleni.
Alisema hayo wakati akifungua kikao kazi kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayotekeleza miradi na afua katika Sekta ya Elimu Novemba 24 2023, Mkoani Arusha.
Mpanju alisema, ni ngumu kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutekeleza miradi yao ikiwa bado watoto wanapitia ukatili au mazingira magumu na kushindwa kusoma.
“Tuwajengee watoto wetu mazingira wezeshi ya kuweza kusoma vizuri na ndiyo mantiki ya kikao cha leo ikiwa ni utekelezaji wa sheria, sera na miongozo ya nchi yetu kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu,” alisema Wakili Mpanju.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kushirikiana na Wizara za kisekta itaanza mara moja kufanyia kazi maazimio ili kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Kaimu Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Grace Mbwilo ametoa rai kwa wadau hao kuwatumia wasajili wasaidizi katika Mikoa yao na Halmashauri ili kurahisisha kazi zao.
“Wasajili wasaidizi waliopo kwenye maeneo yenu wamechaguliwa kwa mujibu wa sheria hivyo msiwaruke, shirikianeni nao kwani kuna baadhi ya changamoto zinaweza kutatuliwa kwenye maeneo yenu bila kuja kwenye ngazi ya Wizara mpaka inaposhindikana kutatuliwa ndiyo mje kwa Msajili wa NGOs,” alisema Grace .
Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Godfrey Boniventura ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa juhudi zake za kuhakikisha inaendelea kuimarisha afua ya elimu ili kupata maendeleo yanayotarajiwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.