HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 katika Kata ya Nzuguni kwa ajili ya kuanzisha mnada wa kuchoma nyama pamoja na kuuza bidhaa nyingine kama vinywaji.
Eneo hilo lipo jirani na soko kuu jipya la Job Ndugai ambapo mnada huo utafanyika kwa siku mbili kwa wiki ambazo ni Ijumaa na Jumapili ambapo wafanya biashara watapatiwa maeneo ya kufanya biashara zao katika eneo hilo mara taratibu za ugawaji zitakapokamilika.
Akizungumza katika eneo hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe aliwaambia wafanyabiashara na wadau wanaofanya shughuli zao katika soko hilo kuwa utaratibu wa ugawaji wa maeneo ya biashara katika gulio hilo utakamilika siku chache zijazo ili gulio lianze.
"Ila niwaambie habari mbaya ndugu zangu, katika eneo hilo hatutaweza kuwapa maeneo ya biashara watu wote wanaohitaji kwa sababu tumegundua mahitaji ni makubwa kuliko eneo letu" alisema Prof. Mwamfupe.
Mstahiki Meya huyo aliwataka wadau hao kuwa na subira wakati Halmashauri inaendelea kufanya utaratibu wa kupata maeneo zaidi yatakayofaa kwa ajili ya wafanyabiashara mbalimbali Jijini humo kufanya kazi zao.
"Tayari Mkurugenzi wa Jiji anayo maelekezo haya na anaendelea kuratibu maeneo zaidi ili kila anayetaka kufanya biashara tumtendee haki" alisisitiza Meya huyo.
Meya huyo alifika katika soko kuu la Job Ndugai akiwa na Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiwa katika ukaguzi wa miradi wa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.