HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imezindua Mpango Mkakati wa kuwawezesha kiuchumi Wanawake na akina Mama wa Manispaa hiyo ili wajikwamue katika changamoto mbalimbali za maisha yao ya kila siku.
Mpango Mkakati huo unaotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018, ulizinduliwa jana Machi 8, 2018 ambapo sherehe za uzinduzi zilienda sambamba na maadhimisho ya kilele cha siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika katika Kata ya Msalato Mjini Dodoma.
Akizindua Mpango Mkakati huo, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Dodoma Fatma Tawfiq alitoa wito kwa Wanawake kuungana na kuwa kitu kimoja ili kupambana na changamoto zinazowakabili ikiwemo za kiuchumi.
Aliwataka pia kuwa tayari kugombea na nafasi mbalimbali za uongozi ili wawe katika nafasi za maamuzi, na kwamba waanze na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwakani kabla ya ule Mkuu wa mwaka 2020.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wa Manispaa ya Dodoma Hidaya Mizega ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika sherehe hizo alisemakuwa, Mpango Mkakati huo ndio dira ya kuwainua wanawake wa Manispaa ya Dodoma kiuchumi na kwamba yataandaliwa majukwaa mbalimbali ya Wanawake ili kuutambulisha kwa wadau.
“Wanawake wataongozwa jinsi ya kuunda vikundi vingi vya kuichumi ili kupata fursa mbalimbali wakiwa pamoja…kwa sasa Dawati la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi limeanzishwa katika kila Kata ya Manispaa ya Dodoma” alisema Mizega.
Alisema kuwa miongoni mwa malengo mahsusi ni kuwa na SACCOS ya akina mama wote wa Wilaya ya Dodoma, hivyo baada ya kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati huo kumalizika, itafanywa tathmini ya kina kuhusu mafanikio na changamoto zilizojitokeza ili zifanyiwe kazi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.