Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Jabir Shekimweri ameagiza ujenzi wa mradi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma unaojengwa kwenye Mji wa Serikali Mtumba ujulikanao kama Government City Compex ukamilike ifikapo tarehe 31 Agosti, 2021.
Shekimweri ametoa maagizo hayo alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa hoteli na kumbi za mikutano eneo la mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma unaogharimu takriban Tsh. Bilioni 18 fedha zitokanazo na mapato ya ndani.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hoteli hiyo itakapokamilika itasaidia kuingiza mapato ya Tsh. Bilioni 1.3 kwa mwaka sawa milioni 108 kwa kila mwezi hivyo unapochelewa kukamilika unapoteza mapato ya Tsh. Milioni 108 kila mwezi na hadi sasa jumla ya Tsh. Milioni 864 zingekuwa zimeshakusanywa kama si kuchelewa ambapo ulitarajiwa kukamilika mwaka jana.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe amesema uharaka wa ujenzi huo usiathiri ubora wa umaliziaji wa jengo hilo huku Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Meja Mstaafu Johnick Risasi akisema suala la mkataba linatakiwa kuangaliwa upya ili kuondoa mkanganyiko pindi panapotokea ucheleweshaji wa miradi.
Awali akitolea maelezo juu ya mradi huo, msimamizi wa ujenzi katika hoteli hiyo ya kisasa mji wa serikali yenye hadhi ya nyota tano, mhandisi Nasri Nasoro kutoka kampuni ya M/S MOHAMMED BUILDERS CO. LTD inayotekeleza mradi huo amesema eneo la kumbi za mikutano, ujenzi umefikia asilimia 90 na upande wa hoteli ukifikia asilimia 75 ambapo kazi inayoendelea sasa ni pamoja na uwekaji wa marumaru.
Naye Mhandisi wa Jiji ya Dodoma QS Ludigija Ndatwa amesema taratibu zote za malipo zilishakamilika katika mradi huo na kilichobaki ni utekelezaji wa kampuni hiyo.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Meja Mstaafu Johnick Risasi akiongea wakati wa ziara hiyo ya viongozi wa Wilaya ya Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.