MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amekutana na kufanya mazungumzo na wasimamizi wa mradi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway-SGR) ofisini kwake Jijini humo ambapo waliutambulisha mradi huo kwa kumuonesha michoro ya jinsi ambavyo stesheni ya Dodoma itakayojengwa eneo la Ihumwa itakavyokuwa.
Ujumbe wa wasimamizi hao wa mradi wa SGR uliongozwa na Naibu Meneja wa mradi huo Mhandisi Chedi Masambaji ambapo pamoja na mambo mengine, alimueleza Mkurugenzi Kunambi kuwa, stesheni ya Reli itakayojengwa Dodoma itakuwa ni ya kipekee kwani haijajengwa kokote dunia.
Masambaji alisema stesheni hiyo itakuwa na maduka makubwa ya kisasa (Malls) pamoja na maeneo ya kuegesha Pikipiki, Bajaji, Teksi, na Mabasi makubwa.
Kutokana na umuhimu wa stesheni hiyo kwa Jiji la Dodoma, Mkurugenzi Kunambi alipendekeza Halmashauri ya Jiji itengewe eneo maalum ndani ya stesheni hiyo litakalotumika kama Kituo cha Habari cha Halmashauri kwa lengo la kupokea wageni mbalimbali na kuwapasha Habari na kuwatambulisha maeneo ya Utalii na Uwekezaji yaliyopo Jijini humo.
“Lakini pia itapendeza kama mtajenga vivuko vya juu katika maeneo ya Wananchi ambapo reli inapita ili kuepuka Wananchi kulazimika kukatiza kwenye Reli” alishauri Kunambi.
Akifafanua hoja hizo, Naibu Meneja huyo wa mradi Mhandisi Masambaji alisema katika mchoro wa mradi huo kwa eneo la Jijini Dodoma yapo madaraja ya juu yatakayojengwa ili kuwarahisishia wakazi wa Dodoma kuvuka kwenye eneo la Reli.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.