KINDA anayekipiga katika Timu ya Dodoma Jiji FC Anuary Jabir ameweka rekodi yake katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2020/2021 kwa kufunga magoli manne ndani ya mechi tatu mfululizo na kuisaidia timu yake kupanda juu ya msimamo wa Ligi hiyo kutoka nafasi ya kumi hadi nafasi ya saba.
Jabir alifunga goli moja katika mechi dhidi ya JKT Tanzania dakika ya 80 ya mchezo akitokea benchi, huku akifunga goli lingine dhidi ya Coastal Union dakika ya 57 na magoli mawili akiyatia kambani dhidi ya Polisi Tanzania mnamo dakika ya 47 na 75 ya mchezo huo.
Akizungumzia rekodi hiyo Jabir amesema siri kubwa ya mafanikio yake ni kujituma, nidhamu, kufanya mazoezi kwa bidii pamoja na kusikiliza kwa makini kile ambacho wanapewa na Mwalimu.
“Nimekua nikitenga muda wangu mwenyewe kufanya mazoezi baada au kabla ya program za mwalimu hiki kimekua kikipandisha kiwango changu kwa kasi na kunifanya nionekane bora uwanjani” Alisema Jabir.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC Mbwana Makata amempongeza Anuary kwa kiwango anachoendelea kukionesha kila anapopewa nafasi huku akimshauri kuwa asibweteke bali aongeze bidii ili kupandisha kiwango chake jambo ambalo linaweza kumpelekea kwenda kucheza soka la kiushindani nje ya nchi.
Aidha, wachambuzi na wataalamu wa masuala ya soka wamempa Jabir nafasi kubwa ya kuchukua Tuzo ya mchezaji bora wa mwezi februari kutokana na kiwango kikubwa alichokionesha katika mzunguko huu wa pili.
Anuary Jabir ndiye aliyekua mfungaji bora wa Ligi Daraja la kwanza na kuisaidia timu yake kupanda Ligi Kuu ila hakuonesha kiwango kizuri mwanzoni mwa msimu jambo lililopelekea kumaliza mzunguko wa kwanza bila goli, na baadaye aliitwa katika kikosi cha Taifa chini ya miaka 20 ambapo hakupata nafasi kubwa ya kucheza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.