MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, amesema kuwa atahakikisha anashirikiana na Waandishi wa habari kwa kuwapa taarifa zote wanazostahili kupata ili ziwafikie Wananchi kwa wakati.
Msigwa ameyasema hayo leo April 16, 2021 Jijini Dodoma wakati wa makabidhiano ya ofisi na mtangulizi wake ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sànaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas.
Aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, leo amekabidhi kijiti hicho kwa Ndugu Gerson Msigwa aliyeteuliwa hivi karibuni na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan huku akikumbuka jinsi kazi hiyo ilivyomfanya asilale.
Dkt. Abbasi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo, pamoja na kazi nyingine, ataendelea kuisimamia na kuisaidia ofisi hiyo ya Msemaji Mkuu, amewaambia waandishi wa habari Jijini Dodoma leo wakati wa makabidhiano kuwa kazi hiyo ilimchukua muda mwingi katika saa 24 za siku hivyo ni kazi adhimu na muhimu kwa Taifa.
Dkt. Abbasi amepongeza Bw. Msigwa kwa uteuzi huo na kueleza kuwa anaamini atafanikiwa kuendeleza pale yeye alipoishia.
Aidha, Dkt. Abbasi amemshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na kumteua mwaka 2016 na amemshukuru pia Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini aendelee kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika uteuzi uliofanyika Aprili 4 mwaka huu.
Pia nawashukuru sana watanzania wote, wanahabari na wahariri wa vyombo vya habari tulioshirikiana katika kipindi chote cha uongozi wangu.
Kwa upande wake, Bw. Msigwa naye alimshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu kwa miaka mitano 5 na zaidi na sasa anamshukuru Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kwenye nafasi ya Msemaji Mkuu wa Serikali.
Vilevile, namshukuru Dkt. Hassan Abbasi kwa kunikabidhi rasmi ofisi leo na kwa kunipa ushirikiano mkubwa wakati nikiwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, ninaamini tuko pamoja hata kwenye majukumu haya mapya, amesema kuwa Dkt. Abbasi katika uongozi wake wa Usemaji Mkuu wa Serikali tayari amefyeka kichaka, na yeye sasa kazi yake ni kulima shamba ili kupata mazao mengi kwa maendeleo ya nchi yetu.
Msemaji Mkuu wa Serikali huyo mpya ameweka wazi kuwa anatamani sana wanahabari wawe chachu ya kuleta mabadiliko, nchi yetu iwe ajenda ya kwanza, tuzingatie sheria, taratibu, kanuni na miongozo ili tuiweke nchi yetu mbele na kuyatangaza mazuri ya nchi yetu.
“Nitakuwa mtu wa mwisho katika kipindi cha uongozi wangu wa Msemaji Mkuu wa Serikali kuona waandishi wa habari tunatumia kalamu zetu kuibomoa Serikali na nchi yetu wenyewe ambayo tayari ilishapata uhuru. Nitahakikisha mnapata taarifa za shughuli zote zinazotekelezwa na Serikali mnazostahili kupata kama waandishi wa habari.”
Aidha, amesema kuwa ataweka mikakati jinsi ya kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji pamoja na wadau wa habari. Akamalizia kwa kumpongeza Dkt. Abbasi kwa kazi kubwa aliyoifanya na leo anakuwa bosi wake ni jambo la kumpongeza sana," alisema Msigwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.