DONDOO ZA YALIYOJIRI WAKATI WA TAARIFA YA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI GERSON MSIGWA, AKIONGEA NA VYOMBO VYA HABARI LEO JUNI 12, 2022 JIJINI DODOMA
Napenda kuwashukuru ndugu zangu waandishi wa habari kwa ushirikiano mkubwa mnaoutoa kwa Serikali katika kutangaza shughuli mbalimbali za Serikali, tunathamini mchango wenu na Serikali itaendelea kushirikiana nanyi wakati wote mtakapohitaji.
Serikali ipo hapa Dodoma, wafanyakazi zaidi ya 18,300 wamehamishiwa hapa Dodoma. Na Serikali inajenga Mji wa Serikali katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma.
Ujenzi wa awamu ya kwanza wa majengo ya Serikali umekamilika kwa asilimia 100 kwa gharamaza ya Shilingi Bilioni 39, hivi sasa tunatekeleza awamu ya pili ambapo tutatumia shilingi Bilioni 621 hadi tutakapokamilisha ifikapo Oktoba mwakani 2023.
Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wanapanda miti 500,000 katika Mji wa Serikali ili kuweka mandhari nzuri ya Ofisi za Umma. Eneo hili la Mji wa Serikali limejengwa barabara nzuri za lami zenye urefu wa kilometa 51.2 na kazi imefikia asilimia 99.
Katika kutekeleza kazi za kuhamia Dodoma, kati ya shilingi Bilioni 621 zilizopangwa, tayari Mhe. Rais ametoa Shilingi Bilioni 300 ambazo sehemu yake ndizo zinatumika katika kazi zinazoendelea hivi sasa.
Mwaka huu wa Fedha Serikali imeidhinisha Shilingi Bilioni 372.6 kwa ajili ya Mkoa wa Dodoma, kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 72 zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko (Ring Road) km 112.3., Uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato, pamoja na miradi mingine ikiwemo maji.
Soko la wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) Dodoma litakuwa pia na huduma muhimu za kibenki, ukumbi wa semina kwa wajasiriamali, ofisi ya machinga, ofisi ya maafisa biashara wa Jiji, eneo maalumu la akina mama kunyonyesha watoto, kituo cha Polisi, huduma ya kwanza, mabucha, maeneo ya mbogamboga matunda, nafaka, nyama choma, baa, saluni za kiume na kike, pamoja na vibanda vya wenye ulemavu.
Sensa ya watu na Makazi
Tutakuwa na Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, kwa sasa maandalizi yamefikia asilimia 88. Mwaka huu tutakuwa na madodoso yafuatayo
Nawaombeni wananchi tulichukue jambo hili la Sensa kuwa la kitaifa kwa umuhimu wa kipekee, tunataka tuandike historia ya kuwa nchi iliyofanya Sensa kwa viwango vya ubora wa hali ya juu na tayari nchi mbalimbali zimeanza kuja kujifunza hapa Tanzania baada ya kupata taarifa juu ya namna tunavyojipanga kutekeleza zoezi hili
Anwani za Makazi
Rais, Mhe Samia Suluhu Hassan aliamua Operesheni ya anwani za makazi itekelezwe kwa miezi 3 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 28 tu badala ya Shilingi Bilioni 700 kama ilivyotarajiwa awali.
Tunawapongeza wote walioendelea kutoa ushirikiano kwenye zoezi la anwani za makazi, nguzo za majina ya mitaa zinawekwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Huduma za Posta
Shirika letu la Posta linaendelea kufanya vizuri na wiki hii tumekuwa na tukio kubwa kwa nchi yetu ambapo Shirika letu la Posta limetiliana saini makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Posta la Oman.
Huko tutaweza kununua na kuuza bidhaa mbalimbali kupitia duka mtandao la Posta Tanzania ambalo linapatikana kwa www.postashoptz.post.
Hivi sasa Posta yetu ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Posta Duniani tayari ina maduka mtandao zaidi ya 800 ambayo mtanzania unaweza kupata bidhaa na unaweza kuuza bidhaa zako, hii ndiyo Tanzania ya Kidijiti
Sekta ya Utalii
Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan anazidi kuimarisha sekta ya utalii, baada ya kurekodi filamu ya Royal Tour idadi ya watalii imeongezeka nchini.
Takwimu kutoka Hifadhi za Taifa (TANAPA) zinaonesha Mwezi Aprili na Mei 2022 idadi ya watalii waliotembelea ni 115,198 (Watalii wa ndani 71,593 na Watalii wa Nje 43,605) ikilinganishwa na Watalii 59,664 (Watalii wa ndani 46,624 na Watalii wa nje 13,040) wa mwezi Aprili na Mei 2021. Ongezeko hili limeongeza mapato kutoka Shilingi Bilioni 5.735 hadi kufikia Shilingi Bilioni 15.559.
Takwimu Hifadhi ya Ngorongoro zinaonesha Mwezi Aprili na Mei 2022 idadi ya watalii imeongeza hadi kufikia 51,044 (Watalii wa ndani 25,150 na Watalii wa nje 25,894) ikilinganishwa na Watalii 22,954 wa Mwezi Aprili na Mei mwaka jana 2021. Hili ni ongezeko la asilimia 122.4.
Mapato kutoka Ngorongoro kwa kipindi hicho nayo yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 2.585 hadi kufikia shilingi Bilioni 10.058. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 289.
Kuhusu Hali ya Loliondo
Serikali inasikitishwa na vitendo vya uchochezi vinavyofanywa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu Loliondo.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella wameeleza kuwa taarifa hizo ni upotoshaji. Hakuna operesheni ya kuwahamisha kwa nguvu wananchi, kinachoendelea ni uwekezaji wa alama za mipaka.
Serikali iko macho, aina yoyote ya uzushi ni kosa kisheria, kwa wanaofanya hivyo watatafutwa na wakipatikana hatua za kisheria zitachukuliwa.
Miradi na Ujenzi
Ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati ya kisasa (SGR) unaendelea na kwa baadhi ya maeneo unakaribia kukamilika, mradi ukifika Kigoma tutaunganisha reli kutoka Uvinza – Msongatin- Gitega (Burundi) – Uvira – Kindu (DRC).
Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere katika mto Rufiji umefikia asilimia 62.95 na unatarajiwa kukamilika Juni 2024.
Ujenzi wa daraja la Magufuli linalounganisha Kigongo na Busisi umefikia asilimia 47.3 na daraja hilo litakuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati, linatarajiwa kukamilika Feb, 2024 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 716.
Ujenzi wa daraja la Wami umefikia asilimia 81.1, ujenzi wake unatarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 71 na litakamilika mwishoni mwa mwezi Novemba 2022.
Ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara umefikia asilimia 57, mradi huu utagharimu shilingi Bilioni 40.44.
Hali ya UVIKO-19
Ugonjwa wa UVIKO-19 bado upo, tunawasihi wananchi kuendelea kuvaa barakoa, kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kufanya mazoezi na kupata chanjo.
Chanjo ya Polio
Nawapongeza wazazi na walezi waliyoitikia wito wa kuchanjwa kwa watoto chanjo ya polio, watoto milioni 12.1 wamechanjwa badala ya milioni 10.2 iliyokadiriwa awali.
Michezo
Nawapongeza Serengeti girls wanaokwenda kuandika historia ya kucheza kombe la dunia, shukrani pia kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na TFF kwa malezi mazuri waliyoyafanya kwa timu hii, wanamichezo wote nchini endeleeni kutumia fursa zilizopo kwenye michezo kwani Serikali imeamua kuiweka kwenye mikakati katika kuitangaza nchi yetu na kutoa ajira kwa vijana.
Serikali imetenga Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga na kuboresha viwanja vya michezo ili wanamichezo wetu wapate maeneo ya kufanyia michezo.
Ujenzi wa meli ni muhimu kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, changamoto zilizokuwa zimejitokeza zinafanyiwa kazi na muda si mrefu meli ya New Mwanza inakamilika.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa (aliyesimama katikati) alipokuwa akingea na Vyombo vya Habari akitoa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali leo tarehe 12 Juni, 2022 Jijini Dodoma.
Imeandaliwa na Idara ya Habari - MAELEZO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.