WASIMAMIZI wasaidizi wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2020 ngazi ya Kata wametakiwa kutunza siri na kuimarisha mawasiliano baina yao na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa ufanisi.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma Mjini, Wakili Msekeni Mkufya alipokuwa akiwasilisha mada ya wajibu, majukumu na mambo ya kuzingatiwa na wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya kata katika mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hivi karibuni.
Wakili Mkufya alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo na kuwaelekeza mambo ya msingi wanayopaswa kuzingatia katika mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. “Mafunzo haya yanatolewa kwenu mkiwa kama wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata kuelekea uchaguzi huo, ambao utafanyika tarehe 28/10/2020. Tukumbuke kwamba, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mchakato wa uchaguzi unatekelezwa kwa mujibu wa sheria, tukianza na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria ya uchaguzi sura ya 343 pamoja na kanuni za uchaguzi wa kiti cha Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2020” alisema Wakili Mkufya.
Akiongelea mambo yanayopaswa kuzingatiwa na wasimamizi wasaidizi wakati wa kutekeleza majukumu yao, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini alisema wanatakiwa kutunza siri. “Kutunza siri kwa maana ya kutokutoa taarifa za uchaguzi kwa mtu au mamlaka zisizohusika. Kuweka utaratibu mzuri wa kuwasiliana na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo, au wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhusu mwenendo wa uchaguzi katika eneo lake” alisema msimamizi huyo.
Mambo mengine ni kuacha ushabiki wa chama chochote cha siasa katika kutekeleza majukumu yao na kufahamu mihemuko ya kisiasa katika eneo lake. Pia, “mnapaswa kukagua na kutembelea vituo vya uchaguzi vilivyopo katika maeneo yenu na mkibaini mapungufu ya vituo, mtafute namna bora ya kurekebisha kasoro hizo kwa kuwasiliana na Msimamizi wa Uchaguzi” aliongeza Wakili Mkufya.
Mambo mengine aliyoyasisitiza msimamizi huyo kwa wasimamizi wasaidizi ni kutetekeleza majukumu yao ya kusimamia uchaguzi kwa kuzingatia uadilifu na uaminifu kwa sababu kukosea ni kuichafua Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kufanya jambo lolote kinyume na sheria na kanuni za uchaguzi ni kosa, kwa mujibu wa kifungu cha 98 cha sheria ya uchaguzi, aliongeza Wakili Mkufya.
Msimamizi huyo wa jimbo aliwataka wasimamizi wasaidizi kuepuka kufanya kazi kasipo kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi au msimamizi wa uchaguzi. Vilevile, aliwataka kuepuka kutokushirikisha msimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika shughuli za uchaguzi katika eleo wanalosimamia.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za mwaka 2020 zinaelekeza chini ya kanuni ya 13 (1) kwamba Tume ya Taifa ya uchaguzi inaweza kuchagua ana kuteua wasimamizi wasaidizi kutoka miongozi mwa watumishi wa umma ambao watakuwa na jukumu la kumsaidia msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo na ngazi ya kata.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.