WANANCHI wa Mtaa wa Ndachi jijini Dodoma wametakiwa kutowasikiliza watu ambao wanachelewesha maendeleo ya mtaa huo kwa kusababisha migogoro ya ardhi kutomalizika mapema kwa maslahi yao binafsi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mheshimiwa Emmanuel Chibago leo alipokuwa akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa huo kwa lengo la kutatua mgogoro ya ardhi.
Naibu Meya Chibago alisema kuwa mgogoro huo umechukua muda mrefu kumalizika kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakichochea mgogoro huo kwa maslahi yao binafsi. Alisema kuwa wengi wa wanaochochea mgogoro huo wanakuwa na maeneo mengine nje na mtaa huo, hivyo, wasiwasikilize kwa sababu wanawacheleweshea maendeleo.
“Ili upate uhalali wa kuwa mmiliki wa ardhi, hati ni muhimu na ndio maana ina mkataba wa muda mrefu wa miaka 99. Ukishapata hati hiyo, unaweza kwenda kukopa kwa sababu unakuwa na umiliki wa ardhi kisheria. Hivyo, ni vyema kutatua mgogoro huu ili kila mmoja aweze kupata haki yake’’ alisema Mhe. Chibago.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango miji na Mazingira ya Halmashauli ya Jiji la Dodoma, Mhe. Jaffari Mwanyemba alisema kuwa wanaelekea ukingoni mwa zoezi hilo. “Ramani pamoja na majina tayari tumeshatoa. Kazi imeandaliwa na wataalamu ambao ni binadamu hivyo, kama kuna kasoro ni vizuri zikatajwa ili kutatuliwa mapema. Kama unaeneo haki haitapotea, tutahakikisha kila mtu anapata haki yake na migogoro kuisha kabisa. Niwasihi tu kufuata vile ambavyo mtakuwa mkiambiwa wakati wa kukamilisha zoezi hilo’’ alisema Mhe. Mwanyemba.
Nae mkazi wa mtaa huo, Sharifa David alipongeza juhudi za halmashauri katika kutatua mgogoro huo uliodumu muda mrefu. Alisema kuwa wanaweza kuendeleza maeneo yao na kujiletea maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.